Wizara ya Madini imekuwa miongoni mwa Wizara zilizoshiriki Kilele cha Kongamano la KURASA 365 za MAMA Vol.III. lililoratibiwa na Clouds Media Group.
Kongamano hilo limehitimishwa leo Machi 27, 2024 jijini Dar Es Salama na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye amezungumzia umuhimu wa Serikali kuendelea kutangaza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika Kongamano hilo, Wizara mbalimbali zimepata wasaa wa kueleza masuala makubwa yaliyofanyika katika Siku 365 za Rais Samia madarakani ikiwemo mikakati ya kuendeleza Sekta hizo.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameileza hadhira iliyoshiriki kuhusu umuhimu wa Sekta ya Madini katika kuchochea uchumi na shughuli nyingine za kiuchumi hivyo kuelezea mikakati ya Serikali kuboresha miundombinu ya barabara ili kuwezesha miradi ya madini kufanyika kwa tija.
Dkt. Kiruswa ametolea mfano ujenzi wa barabara itakayowezesha usafirishaji wa madini katika kiwanda kikubwa na cha aina yake cha kusafisha madini ya metali yakiwemo Madini ya nikeli kinachotarajiwa kujengwa Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga ambapo hivi karibuni Serikali ilitoa Leseni ya kiwanda hicho.
” Mikakati ya Serikali ni kuunganisha barabara ya kwa Msisi Handeni ili kuiunganisha na barabara ya Tanga Dar Es Salaam kuweza kusafirisha Madini ya Kinywe yanayochimbwa na Mtanzania GodMwanga,” amesema Dkt. Kiruswa.
Akizungumzia ukuaji wa Sekta ya Madini, Dkt. Kiruswa amesema kumekuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa Sekta ya Madini hali inayodhihirisha kufikiwa kwa malengo ya kufikia asilimia 10 ya mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato laTaifa ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyoanishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Aidha, Dkt. Kiruswa amebainisha mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuwaendeleza na kuwainua wachimbaji wadogo wa madini nchini ikiwemo kuweka tozo ndogo ili kuwawezesha wafanye shughuli zao kikamilifu na hivyo kuchangia mapato ya Serikali.
Post A Comment: