Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amesema atafanya ziara ya kutoa elimu ya lishe kijiji kwa kijiji na hasa katika maeneo qmbayo yameonekana kuathirika zaidi na tatizo la udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano ili kuhakikisha tatizo hilo linamalizika katika wilaya yake.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya takwimu za wilaya hiyo kuonyesha zaidi ya 47% ya watoto walio chini ya miaka mitano wilayani Ludewa wanakabiliwa na tatizo hilo la udumavu kitu ambacho hakipaswi kuwepo kwa kiwango hicho kwakuwa wilaya hiyo ina uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na matunda.

“Ludewa tunazalisha vyakula vya kila aina ambavyo ni mtaji tosha katika kuhakikisha watoto wetu wanapata afya bora na kuondokana na udumavu, mimi na timu yangu tutapitakitoa elimu kila kona ya wilaya hii na kuhakikisha tatizo hili linakwisha”. Amesema Mwanziva.

Aidha kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratius amesema kupitia mapato ya ndani ya halmashauri hiyo imetenga fedha kiasi cha sh. Mil 33 zilizolenga kuchangia uboreshaji wa huduma ya lishe kwa watoto wilayani humo sambamba na uandaaji bustani za mboga mboga na matunda katika shule zote za msingi na sekondari.

Awali afisa lishe wa Ludewa John Kiussa akitoa takwimu za udumavu huo mbele ya mgeni rasmi mkuu wa mkoa huo Antony Mtaka katika mkutano wa hadhara wa utoaji elimu ya lishe amesema miongoni mwa sababu zinazopelekea kuwepo kwa udumavu kwa watoto hao kuwa ni ulevi uliokithiri pamoja na mama kuanza kufanya shughuli za kilimo mapema na kupelekea kukosa muda wa kumpa mtoto huduma stahiki.

Hali hiyo imepelekea mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka kutoa rai kwa wananchi wote wa mkoa huo kuacha unywaji pombe uliokithiri lakini pia kujifunza kwa makabili mengine namna ya kuhudumia akina mama waliojifungua kwa kuanza shughuli za kiuchumi baada ya miezi mitatu ya kujifungua badala ya wiki moja kama ambavyo wengi wao hufanya.

” Unakuta mama katoka kujifungua tuu ndani ya wiki anaenda shambani anamuweka mtoto chini ya mti wakati yeye akilima, sasa kwa mazingira hayo mnategemea huyo mtoto ananyonyeshwa na kuandaliwa lishe bora saa ngapi!?”. Amesema Mtaka.

Sanjali na hilo pia amewataka wazazi kuacha kuwalisha watoto viporo vya chakula ikiwemo viporo vya kande na kuwanyamazisha kwa kuwanywesha pombe ili walale usingizi kwani kwa kufanya hivyo ni kuwaharibu watoto kiafya na kiakili.

Naye mganga mkuu wa Mkoa wa Njombe Juma Mfanga amesema mkoa wa Njombe umetajwa kuwa nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 50.4 ya uwepo wa watoto wenye udumavu chini ya umri wa miaka mitano huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na mkoa wa Iringa ambao una asilimia 56.9.




Share To:

Post A Comment: