Mkuu wa Wilaya ya Ludewa- Victoria Mwanziva akiambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias na Wataalam wa Idara ya Kilimo Wilaya ya Ludewa- wametembelea Kiwanda cha City Coffee kilichopo Mbeya- kwa ajili ya kikao kazi cha kuongeza tija kwenye zao la Kahawa Wilayani Ludewa.

Wilaya ya Ludewa kwa Mwaka 2023/2024 imezalisha Jumla ya Tani 150 za Kahawa na sasa inakwenda kwenye mkakati makhsusi wa kuzidi kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao hili la kimkakati.

Ziara hii imehusisha kutembelea Shamba la Kahawa la Utengule-Mbeya kwa ajili ya kujifunza teknolojia za kisasa za uzalishaji Kahawa na uzalishaji wa miche bora. 

Akizungumza mbele ya viongozi Mkuu wa Wilaya ya Ludewa amesema, Kahawa ni zao la biashara ambalo lina uwezo wa kuzidi kuinua Uchumi wa Mkulima, Wilaya na Taifa kwani Ludewa ina mazingira bora na eneo lote linalofaa kwa uzalishaji wa zao la kahawa ni hekta 21,300. 

Katika hatua nyingine Mhe Mwanziva ameeleza kwamba Wilaya ya Ludewa ina Vitalu vinane (8) vya kuzalisha miche bora ya kahawa ikiwa ina vyama vya ushirika vya wakulima wa zao la kahawa viwili (2) ambavyo ni Ludewa Coffee Growers na Mawengi Coffee Growers. Vyama hivi vina mashine za kumenyea kahawa (CPU’s). 

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Ludewa ameongeza kwamba Mikakati ya kuzidi kuhuisha zao hili ni pamoja na: Kutoa Mafunzo zaidi kwa Wakulima, Ma-Afisa Ugani na Vyama Vya Ushirika, Kuongeza Ubora wa Kahawa, Kuongeza Tija kwenye Uzalishaji, Kuongeza teknolojia ya uzalishaji miche bora ya Kahawa. 

Mwisho Dc Mwanziva amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye zao la Kahawa Wilayani Ludewa. 










Share To:

Post A Comment: