Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imefanya ziara wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, Machi 27, 2024 kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Akizungumza baada ya kukagua miundombinu ya umeme katika Zahanati ya Magodi, Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu ametoa wito kwa viongozi mbalimbali ngazi ya Wilaya, Vijiji na Vitongoji nchini kote kuhamasisha wananchi waliofikiwa na umeme wa REA kuchangamkia fursa ili waunganishiwe nishati hiyo.
“Serikali imebeba mzigo wa gharama zote na hivyo wananchi wanatakiwa kulipia VAT ambayo ni shilingi 27,000 tu. Tushirikiane kuwahamasisha wachangamkie fursa za miradi ya REA maana miradi hiyo ikishakabidhiwa kwa TANESCO watalazimika kulipa gharama zilizowekwa ambazo ni sawa na Mjini,” amefafanua.
Aidha, akishirikiana na Wajumbe wa Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), walichangia shilingi laki tano kusaidia baadhi ya taasisi za umma na wananchi waliofikiwa na umeme ili waunganishiwe huduma hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa eneo hilo akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji Rashid Banda, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Magodi, Zuwena Mohamed na Mzee Athumani Athumani wamempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Nishati pamoja na REA kwa kufikisha umeme katika kijiji hicho jambo ambalo wamesema limeleta mabadiliko makubwa kimaendeleo.
Katika ziara hiyo, Bodi imekagua pia Mradi wa Umeme wa Vijiji-Miji (Peri-Urban) katika kitongoji cha Mtandikeni, kijiji cha Duga Mafoloni ambapo Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo ameahidi kukamilisha kazi ifikapo mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.
Bodi ya Nishati Vijijini iko mkoani Tanga kushiriki vikao vya kazi na inatumia fursa hiyo kutembelea miradi mbalimbali ya umeme vijijini kujionea maendeleo yake.
Post A Comment: