Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha huduma cha Masista wa Shirika la Dada Wadogo kinachotarajiwa kujengwa eneo la Bagamoyo ambapo jumla ya kiasi cha Shilingi Milioni 237 imekusanywa.
Harambee hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 5 Januari, 2024 katika ukumbi wa Marantal Msimbazi Centre ambapo pamoja na mambo mengine lengo kuu lilikuwa ni kukusanya Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Waziri Bashungwa amelipongeza Shirika hilo kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwatia moyo kuwa ataendelea kushirikiana nao katika zoezi hilo la Ujenzi wa Kituo hicho.
Viongozi Wakuu waliochangia katika Harambee hiyo ni pamoja nana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista J. Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila pamoja na Viongozi wengine wa Serikali.
Aidha, Waziri Bashugwa kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama wameeahidi kuendelea kushirikiana bega kwa bega na Shirika hilo katika ujenzi wa kituo hicho hadi kitakapokamilika
Akisoma Risala, Kiongozi wa Mradi kutoka Shirika la Dada Wadogo Mtakatifu Francisko (Little Sister of St. Francisko), Sista Bahati Leah ameeleza kuwa Shirika hilo kwa upande wa Tanzania wanafanya utume katika majimbo manne ikiwemo Jimbo kuu la Arusha, Same, Shinyanga, Morogoro naBagamoyo.
Ameeleza kuwa Shirika hilo linatoa huduma mbalimbali zikiwemo huduma za kiroho, kimwili, kusaidia walemavu, masikini, vipofu, wazee, wagonjwa na watoto walioko kwenye mazingira hatarishi.
Naye, Mhasibu Mkuu kutoka Taasisi za Marian Bagamoyo, Padre Felix Jabu, ametoa ahadi kwa niaba ya Taasisi hiyo kuwa itatoa tofali zote zitakazotumika katika ujenzi wa Kituo hicho, Mchanga, Kokoto pamoja na mafundi ujenzi wa kituo hicho.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ujenzi wa Kituo hicho Bw. Benard Kileghe amesema kuwa zoezi hilo lilianza mwezi wa 11, 2023 likiwa na lengo la kupata kituo kikubwa cha Huduma cha Bagamoyo kitachotoa huduma kwa wahitaji na wahudumu wa Shirika hilio.
Miongoni mwa walioshiriki harambee hiyo ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Jonas Mpogolo, Diwani kata Nyabiyonza kutoka Karagwe, Thomas Rwentabaza pamoja na Kwaya ya Makuburi.
Shirika la Dada Wadogo Mtakatifu Francisko ni Shirika la Jimbo Katoliki ambalo lilianzishwa mwaka 1923 huku makao yake makuu yakiwa nchini Uganda na mpaka sasa lina wafuasi 800 wanaofanya utume katila nchi nne Uganda, Kenya, Tanzania na Marekani (USA).
Post A Comment: