WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amewataka viongozi wa wakala wa huduma za misitu Tanzania kuchukua hatua stahiki kwa ofisa askari wa uhifadhi wasio na maadili.
Kairuki amezungumza hayo katika hafla ya uzinduzi wa vitendea kazi vya doria za misitu ambapo jumla ya vifaa vilivyokabidhiwa ni 43, magari 2 aina ya Kamaz magari mawili aina ya Land cruiser hard top na pikipiki 39 aina ya Yamaha zenye uwezo mkubwa katika utendaji kazi
Amewataka maofisa na askari uhifadhi kutumia vifaa hivyo kwa malengo na kazi zilizokusudiwa za doria na usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki.
“Kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha utendaji wa jeshi letu leo tunashuhudia jitihada za Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kuboresha mazingira ya utendaji kwa kununua vitendea kazi hivi ambavyo ni magari maalum mawili yenye kuweza kutoa huduma hususani doria katika mazingira magumu ya msituni na pikipiki 39 zenye uwezo wa juu kiutendaji” Kairuki amesisitiza.
Waziri Kairuki ameielekeza TFS kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinatunzwa ili viweze kutoa huduma bora kwa muda mrefu, TFS iweze kuonyesha mabadiliko ya usimamizi wa misitu, rasilimali nyuki na usimamizi wa mashamba ya miti nchini na kuimarisha utekelezaji wa shughuli za jeshi la uhifadhi kwa ujumla.
Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kupunguza matumizi ya mkaa na kuni na kutumia nishati mbadala kama vile mkaa mbadala (briquattes), gesi ili kunusuru uharibifu wa misitu na pia kujiepusha na uvamizi katika maeneo yote yaliyohifadhiwa iwe ni misitu, au maeneo ya hifadhi za wanyamapori.
Katika hatua nyingine, Kairuki amewataka maafisa na askari wote wa jeshi la uhifadhi kujiepusha na vitendo vya rushwa, uzembe na hujuma zote za mali za umma wakati Serikali inajitahidi kuboresha mazingira ya utendaji, maslahi ya watumishi na kuboresha mifumo
“Mnatakiwa kufanya kazi kwa weledi na ari ya hali ya juu kwani Serikali ya Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan inatambua kazi na dhamana kubwa mliyokabidhiwa” Kairuki amesema.
Waziri Kairuki amewahakikishia moafisa na askari uhifadhi kuwa Serikali itaendelea kuboresha utendaji kazi wao kwa kuwapatia vifaa na taaluma muhimu zinazohitajika ili kuleta matokeo chanya katika uhifadhi wa misitu.
Hafla hiyo pia iliambatana na kukabidhiwa na kuzinduliwa kwa magari madogo mawili (2) ambayo yamenunuliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) kwa ajili ya kusaidia jitihada za Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania katika kujenga uwezo wa kusimamia misitu yetu kwa ufanisi.
Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo amesema vifaa vilivyozinduliwa vitaimarisha jitihada za usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki nchini.
Post A Comment: