Waziri wa Madini Anthony Peter Mavunde amesema Serikali kupitia Tume ya Madini itaendelea kusimamia manunuzi ya bidhaa na huduma kwa kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa watanzania kwa mujibu wa Sheria ya Madini,Sura ya 123.
Mavunde ameyasema hayo leo Jijini Mwanza wakati akifungua kiwanda cha ukarabati wa mitambo uchimbaji na uchorongaji kinachoendeshwa chini ya ubia wa Kampuni ya SANDVIK ya Sweden na JC GEARS GROUP LTD cha Tanzania.
“ Kazi kubwa imefanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kunakuwepo na mazingira mazuri ya uwekezaji na hivyo kuvutia ushiriki wa kampuni kubwa za Madini katika mnyororo mzima wa thamani kwenye sekta ya madini.
Kwa kuzingatia hilo Serikali ilifanya mabadiliko kwenye sheria ya Madini mwaka 2017 yaliyopelekea kutungwa kwa kanuni za ushirikishaji wa Watanzania za mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti ya ushiriki wa watanzania kwenye sekta ya madini.
Matunda ya Kanuni ni hapa leo kwenye ufunguzi wa kiwanda cha kukarabati mitambo ya hudum za madini ambacho kinamilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Kitanzania na ya Sweden.
Huu ndio muelekeo ambao serikali itauchukua kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanashiriki katika sekta ya madini.
Miaka michache iliyopita huduma na bidhaa migodini zilikuwa zinapatikana nje ya nchi kwa asilimia zaidi ya 90,kwasasa tunaendelea kuwajengea uwezo watanzania ili haya yote yafanyike ndani ya nchi kwa asilimia kubwa”Alisema Mavunde
Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JC GEARS GROUP LTD Ndg. James Makanyaga amesema mabadiliko ya sheria ya Madini yameongeza ushiriki wa watanzania kwenye uchumi wa sekta ya madini kwa kiwango kikubwa na pia yamechochea upatikanaji wa Ajira kwa watanzania.
Post A Comment: