NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka wananchi wa Kijiji cha Goka kuacha kujiunganishia maji kwenye bomba kuu linalopeleka maji kwenye tenki, kwani kufanya hivyo, kunawanyima fursa ya kupata maji wananchi wa vijiji vingine vitano vya Kata ya Rangwi.
Wananchi hao wametoboa bomba kuu na kuchukua maji kwa nguvu kwa ajili ya matumizi ya kunywa na kunyweshea mashamba yao kwa madai kuwa chanzo cha maji hayo kipo kwao lakini mtandao wa mabomba unakwenda kwa vijiji vingine.
Mahundi amesema hayo Januari 9, 2024 alipokuwa anazungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Emau, Kata ya Rangwi, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
Ambapo ameeleza kuwa hakukuwa na sababu wananchi hao kujiunganishia maji kwenye bomba kuu linalopeleka maji kwenye tenki badala yake wangeomba kuwekewe miundombinu ya maji ikiwemo mabomba na vituo vya kuchotea maji (vilula), lakini baada ya maji yote kuingia kwanza kwenye tenki.
“Wananchi wa Goka msiwe wabinafsi kwa kujiunganishia maji kutoka kwenye bomba kuu kabla ya kuingiza maji kwenye tenki,mnatakiwa mruhusu maji yafike kwanza kwenye tenki ambapo vijiji vyote sita vya Kata ya Rangwi ikiwemo Emau, Rangwi, Nkelei, Karumele, Goka na Mambo vitapata maji,”amesema Mahundi.
Pia amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Goka kwa kuweza kukilinda chanzo hicho cha maji tangu kujengwa kwa mradi huo miaka 46 iliyopita huku akitaka waongeze jitihada za kukitunza sababu bomba lililowekwa na CHAMAVITA, chanzo kina maji mengi, lakini lilipo bomba kuu, chanzo kimepungua.
Aidha ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kumtua mama ndoo kichwani itahakikisha ifikapo mwaka 2025, wananchi wa vijijini watapata maji kwa asilimia 85 huku mijini wakipata kwa asilimia 95.
Awali Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga amesema baada ya kusikia wananchi wamejiunganishia maji kutoka kwenye bomba kuu linalopeleka maji kwenye tenki, walikwenda na askari wenye bunduki ili kung’oa mabomba yote yaliyounganishwa.
“Baada ya zoezi hilo kumalizika, ilibidi turudi kuja kuomba radhi,kumbe kile kitendo kiliwaudhi wazee sababu tangu Uhuru, hawajawahi kupelekewa askari wenye bunduki,sasa hivi wamerudi tena kujiunganishia maji kwenye bomba kuu linalopeleka maji kwenye tenki,”amesema Mhandisi Sizinga.
Mhandisi Sizinga amesema kutokana na maji kuchukuliwa njiani kabla ya kufika kwenye tenki, inasababisha mgao mkali sababu presha ya maji yanayoingia kwenye tenki ni ndogo.
Akiwa Kijiji cha Masereka, Kata ya Mbaru, Mahundi aliwaeleza wananchi wa kata hiyo kuwa anafahamu shida ya maji walionayo wananchi wa kijiji hicho hivyo wataweza kupeleka maji kwa njia mbili, kwanza kwa kutumia chanzo cha maji Goka, ama kuchimba visima, kuweka kwenye matenki na kusambaza maji hayo kwa mtandao wa mabomba.
Post A Comment: