Na OKULY JULIUS , Dodoma

SHIRIKA la Amend kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania wametoa mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda zaidi ya 250 katika Jiji la Dodoma , lengo ni kuliepusha kundi hilo pamoja na watumiaji wengine wa barabara dhidi ya ajali za barabarani.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyohusisha pia wadau mbalimbali, Meneja wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo amesema wametoa mafunzo hayo kwa kutambua kuwa ajali za barabarani zimekuwa chanzo kikubwa cha ajali na ajali nyingi zinatokana na uendeshaji usizingatia usalama barabarani.

“Ajali za barabarani ni sababu kuu ya vifo vya watoto na vijana kati ya miaka 5 na 29 ulimwenguni. Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara lina viwango vya juu zaidi vya vifo vya barabarani duniani.

“Takwimu zilizochapishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni zinaonyesha zaidi ya waendesha pikipiki 3,700 walikufa kwenye barabara za Tanzania mnamo 2016(mwaka wa hivi karibuni ambao data kamili zinapatikana).

“Hii ni sawa na kiwango cha vifo vya waendesha pikipiki cha 67 kwa kila watu 100,000 -mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya vifo vya pikipiki barani Afrika,”amesema Kalolo.

Ameongeza pamoja na kusababisha ajali kwa madereva na abiria wake, pikipiki pia husababisha hatari kwa watumiaji wengine wa barabara, haswa watembea kwa miguu.

Amesema kwa bahati nzuri hatua madhubuti za kuzuia ajali za barabarani zinafahamika, zikijumuisha elimu ya kina kwa watembea kwa miguu na mafunzo ya usalamabarabarani kwa waendesha pikipiki, ambayo yametolewa chini ya mradi huu.

“Jijini Dodoma, Ubalozi wa Uswisi umefadhili utoaji mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki (boda-boda) 250. Mradi huu wa mafunzo ya pikipiki umeandaliwa mahususi kwa waendesha pikipiki na mazingira ya Tanzania.

“Muundo wa mafunzo hayo unatokana na mafunzo ya msingi ya lazima ya Uingereza kwa waendesha pikipiki, lakini umetoa nafasi kwa wakufunzi wa Kitanzania kuyarekebisha ili kukidhi mahitaji halisi ya hapa nchini.

“Mafunzo hayo yalitoa elimu ya vitendo iliyolenga kujenga uwezo ambao madereva wengi wa pikipiki wanajulikana kuukosa. Mazoezi ya vitendo yalijumuisha matumizi sahihi ya makutano na mizunguko, kuvuka vyombo vingine vya moto kwa usalama, na jinsi ya kusimama haraka katika dharura,”amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Amend katika kufanikisha utolewaji wa mafunzo ya usalama barabarani katika mikoa mbalimbali ukiwemo wa Dodoma.


Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Afya katika Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania Viviane Hasselmann amesema  kuwa asilimia 62 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 25, ni muhimu kuelekeza afua za maendeleo kwa vijana, na kushughulikia changamoto na mahitaji yao mahususi.

“Kupitia mradi huu, na mafunzo haya ya pikipiki, Ubalozi wa Uswisi kwa kushirikiana na Amend, wanalenga kuboresha usalama wa waendesha pikipiki, abiria na watumiaji wengine wa barabara, na hivyo kuzuia vifo na majeruhi wengi vijana kadri inavyowezekana,”amesema.


Akizungumza mbele ya wadau wa usalama barabarani Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweli ametoa shukrani kwa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania kwa kufadhili mafunzo hayo kwa waendesha bodaboda kwani yanachangia kupunguza ajali za barabarani nchini.

Amesema kuwa katika mwaka 2023 watu zaidi ya milioni 61 wamefariki duniani na kati hayo waliofariki kwa ajali za barabarani ni watu zaidi ya milioni moja na hiyo ni picha ya dunia.

“Tukiangalia kwa Tanzania Jeshi la Polisi liliripoti makosa ya barabarani 2534 kwa mwaka mzima na ajali za barabarani zilizokuwa zimetolewa taarifa 1760 lakini vifo vilivyotokana na hizo ajali ni vifo zaidi ya 1000 kwa maana katika kila ajali tatu kuna mtu mmoja alikufa.

“Kwa Dodoma hali inasura inayofanana na hiyo , imeripotiwa ajali zaidi ya 1000 na kati ya hao 59 wamefariki dunia.Na hizo ni taarifa ambazo zimeripotiwa na jeshi la polisi.Kwa hiyo mafunzo haya yana umuhimu wa kipekee,”amesema Shekimweri.

Amesisitiza ajenda ya mafunzo ya elimu ya usalama barabarani yanaumuhimu wa kipekee kwani mbali ya vifo ajali hizo zinasababisha ulemavu wa kudumu huku akieleza takwimu za sensa zinaonesha asilimia kubwa ya watanzania ni vijana na kutokana na changamoto za ajira watu wengi wameamua kujikita katika ujasiriamali na bodaboda.

Amesisitiza kuwa ili kuendelea kukomesha ajali za barabarani iko haja kwa Amend, Ubalozi wa Uswisi na wadau wengine kuendelea kutoa mafunzo kwa kundi hilo la waendesha bodaboda huku akitoa rai kwa waendesha bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Awali Mkuu wa Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi Michael Deleli amesema watumiaji wengi wa bodaboda walihama kutoka katika kuendesha baiskeli, hivyo mafunzo hayo ni muhimu kwao.

“Wengi wetu tunaendesha pikipiki kwa uzoefu wa baiskeli hivyo wengi hawakupitia mafunzo rasmi ya udereva.Sisi kama Jeshi la Polisi tunaendelea kupongeza wadau ambao wanajitolea kutoa mafunzo kama haya, kwetu inakuwa furaha kubwa.

Amesema mafunzo ambayo wamefundishwa ni vema wakayapeleka na kwa watumiaji wengine ambao hawajahudhuria mafunzo hayo ili wote wawe salama huku akielezea umuhimu wa kuvaa kofia ngumu kwani ndio usalama wa mhusika.

“Usipovaa kofia ngumu ukianguka sehemu kubwa ya mwili ambao unaumia na hasa ukiwa spidi ni kichwani.vifo vingi vya pikipiki ni kuangukia sehemu ya kichwa, kwa hiyo tusipovaa kofia ngumu maisha yanakuwa hatarini,hivyo nisisisitize wote tunapokuwa katika bodaboda tuvae kofia ngumu.”
Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: