Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt.Eblate Ernest Mjingo amesema Taasisi hiyo imeanza rasmi zoezi la kuwatoa Tembo mikanda ya visukuma mawimbi (GPS Collars ) katika Wilaya za Longido, Hanang, Babati, Monduli ambapo kuna shoroba za wanyamapori zilizopitiwa na mradi wa Njia ya Umeme ya Msongo wa kV 400 wa Kenya - Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP).
Akizungumza Wilayani Longido, Dkt.Mjingo ameeleza kuwa katika Mradi wa KTPIP unaokatiza maeneo ya Shoroba za wanyamapori za Tanganyeeti na Laasarack Wilayani Longido, Ushoroba wa Kwakuchinja Wilayani Babati, Mswakini chini Wilayani Monduli na Pori la akiba la Swagaswaga, TAWIRI imefanya tafiti na kuishauri Serikali kupitia TANESCO ili kuwa na uhifadhi endelevu nchini.
" ili kupata taarifa za kisayansi ,njia mbalimbali za kitafiti zimeendelea kutumika katika mradi huu ambapo mwaka 2019 tuliwafunga Tembo 30 GPS Collars katika shoroba hizo kwa lengo la kufuatilia kama wanyama wataendelea kupita baada ya kutekeleza mradi. Matokeo ya awali yameonyesha wanyama wameendelea kupita hata baada ya miundombinu kusimikwa na ufuatiliaji unaendelea pale umeme utakapowashwa " amefafanua Dkt. Mjingo
Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Marco Ng'umbi, wakati wa kuwatoa Tembo GPS collar Wilayani humo, amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi shupavu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inahakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu nchini, ambapo katika kuwaletea watanzania maendeleo kupitia miradi ya kimkakati inafanya tathimini ya athari za kimazingira na kijamii ambapo hupata ushauri sahihi wa kisayansi kupitia tafiti.
Naye, Mhandisi John Lazimah kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambaye pia ni Mhandisi mazingira katika Mradi huu wa (KTPIP ), amesema mradi huo unaunganisha Nchi za Kenya na Tanzania unalenga kuunganisha mfumo wa umeme wa Nchi za Afrika Mashariki ( Eastern African Power Pool) na kuziwezesha nchi hizi kuuziana umeme, kwa Tanzania mradi unatekelezwa kutoka Singida hadi Namanga kupitia kituo cha kupooza umeme cha Lemugur- kilichopo Kisongo Mkoani Arusha.
Aidha, Mhandisi Lazimah amebainisha kwamba Tanzania inaendeleaa kukua kiuchumi kupitia mradi wa KTPIP kwa kuzalisha umeme wa ziada na kuuza kwa nchi nyingine, Pia kuwa na umeme wa uhakika kunapokuwa na uzalishaji mdogo wa umeme nchini kutokana na sababu zisizo epukika, nchi inaweza kununua kutoka nchi nyingine na kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea umeme kufanyika bila kuathirika.
Kwa mujibu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mradi huu wa Kenya -Tanzania Power Interconnection Project unagharimu kiasi cha Dola za kimarekani 258 Milioni na unatarajiwa kukamilika mapema mwaka huu.
Post A Comment: