Jumuiya ya Kampuni za Kuongoza Uwindaji wa Kitalii Tanzania (Tanzania Hunting Operators Association-TAHOA) imeendelea kutoa mkono wa pole kwa jamii ya Wana Hanang waliopatwa na maafa ya mafuriko yaliyotokea mwezi Desemba mwaka jana ambapo leo imekabidhi mabati 1143 ikiwa ni mchango wa vifaa vya ujenzi.
Mchango huo wa mabati unakuja ikiwa ni mwendelezo wa TAHOA kutoa mkono wa pole kwa Wana Hanang ambapo awali ilichangisha fedha takribani shilingi za kitanzania milioni 47 na kuzikabidhi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb)
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo leo Januari 11, 2024 Wilayani Hanang Mkoani Manyara Katibu Mkuu wa TAHOA, Suleiman Masato amesema kuwa TAHOA imeguswa na maafa hayo huku ikiahidi kuendelea kutoa michango mbalimbali ili kuwagusa Waathiriwa hao.
“Leo tumekabidhi jumla ya mabati 1143 yenye geji 28 mita 3 ambayo ni kiwango kinachokubalika na Serikali”amesema Masato.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mhe. Janeth Mayanja ameishukuru TAHOA kwa kuguswa na matatizo yaliyotokea Wilayani Hanang na kwa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwajengea makazi bora wananchi wa Hanang.
“Mchango huu mliouleta umegusa maisha ya wananchi wa Hanang waliopata madhara ya mafuriko kama tunavyojua wengine wamepoteza makazi na vifaa mbalimbali na nafahamu mlitanguliza kutoa mchango wa fedha katika akaunti ya maafa lakini leo mmekuja kwa mara nyingine hapa Hanang kwa ajili ya kuleta vifaa vya ujenzi, hivyo kwa niaba ya Serikali nawashukuru sana”amesema Mhe. Mayanja.
Post A Comment: