Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza baada ya kuzindua Baraza la Veterinari Tanzania awamu ya sita jijini Dodoma ambapo amewataka maafisa mifugo nchini kufanya kazi za udaktari wa mifugo walizosomea na kuwatembelea wafugaji badala ya kuwa wakusanya mapato wa halmashauri.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifuo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amebainisha kuwa ana imani maafisa mifugo ambao walikuwa wakituma maombi kwa ajili ya kusajiliwa kwenye Baraza la Veterinari Tanzania sasa wataanza kusajiliwa rasmi kwa kuwa baraza hilo tayari limezinduliwa. Prof. Shemdoe amesema hayo wakati wa uzinduzi wa baraza hilo awamu ya sita.
Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari Tanzania Prof. Lughano Kusiluka akizungumza wakati wa uzinduzi baraza hilo awamu ya sita jijini Dodoma ambapo amesema baraza limekuwa likisimamia sheria za veterinari kwa kuhakikisha wataalamu wanaohusika na kutoa huduma za afya za wanyama wafugwao na wasiofugwa wanafanya kazi kwa kufuata sheria na maadili.
Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania Dkt. Amani Kilemile akitoa neno la shukran pamoja na maelezo mafupi juu ya wajumbe wa baraza ambao wameteuliwa watakaodumu kwa miaka mitatu wakati wa uzinduzi baraza hilo awamu ya sita jijini Dodoma.
Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe, Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari Tanzania Prof. Lughano Kusiluka, Msajili wa baraza hilo Dkt. Amani Kilemile pamoja na wajumbe wa baraza hilo baada ya kuzinduliwa rasmi jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Na. Edward Kondela
Maafisa mifugo nchini wametakiwa kufanya kazi za udaktari wa mifugo walizosomea na kuwatembelea wafugaji badala ya kuwa wakusanya mapato wa halmashauri.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amebainisha hayo mjini Dodoma wakati akizindua Baraza la Veterinari Tanzania awamu ya sita baada ya baraza hilo kupata wajumbe.
Mhe. Mnyeti amesema baadhi ya maafisa mifugo wamekuwa wakijikita zaidi kwenye kukusanya mapato ya halmashauri minadani badala ya kuwatembelea wafugaji ili kujua matatizo yao.
“Maafisa mifugo kwenye halmashauri wanajifanya watumishi wa halmashauri kwa ajili ya kukusanya mapato kwenye minada kukusanya ushuru wa ng’ombe badala ya kufanya kazi za udaktari na kuwatembelea wafugaji.” Amesema Mhe. Mnyeti
Aidha, amelitaka Baraza la Veterinari Tanzania kuhakikisha linachukua hatua zaidi kwa maafisa mifugo ambao wamekuwa wakifanya kazi kinyume na maadili pamoja na kuwapatia semina mara kwa mara ili kuwakumbusha wajibu wao kwa wananchi.
Amesema pia ifike wakati maafisa mifugo ambao wanakiuka maadili wafukuzwe kazi pamoja na kufutiwa leseni zao ili kazi hiyo ifanywe na watu ambao watafuata taratibu na maadili ya kazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifuo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema ana imani maafisa mifugo ambao walikuwa wakituma maombi kwa ajili ya kusajiliwa kwenye Baraza la Veterinari Tanzania sasa wataanza kusajiliwa rasmi kwa kuwa baraza hilo tayari limezinduliwa.
Amefafanua kuwa amekuwa akipata ujumbe kwa njia ya simu kutoka kwa baadhi ya maafisa mifugo ambao wamekuwa wakihitaji kusajiliwa lakini hawakuweza kusajiliwa kwa kuwa baraza halikuwa na wajumbe.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari Tanzania Prof. Lughano Kusiluka amesema baraza limekuwa likisimamia sheria za veterinari kwa kuhakikisha wataalamu wanaohusika na kutoa huduma za afya za wanyama wafugwao na wasiofugwa wanafanya kazi kwa kufuata sheria na maadili.
Ameongeza kuwa kazi kubwa ya baraza ni kuwaandikisha na kuwaingiza kwenye daftari la baraza hilo na kufuatilia kiwango na huduma wanazotoa, kusimamia elimu ya wanyama inayotolewa na taasisi mbalimbali na kufuatilia kwa ukaribu wadau wapate huduma inayotakiwa.
Baraza la Veterinari Tanzania awamu ya sita lililozinduliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti litadumu kwa miaka mitatu.
Post A Comment: