Na Said Mwishehe 


KABLA sijahau naomba nieleze jambo kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Mara Said Mtanda kwa kauli yake aliyoitoa kuhusu waandishi wa habari.

Mtanda ametoa kauli kuzungumzia malipo ya waandishi wa habari wanaofanya kazi na Mkuu wa Mkoa, akaweka wazi hadhi ya Mkuu wa Mkoa kwamba italindwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Wakati akielezea hadhi ya Mkuu wa Mkoa akatoa na kiwango ambacho Mwandishi wa habari atakayefanya naye kazi anastahili kulipwa.Ndio Mtanda ametamka hadharani.

Ametoa maelekezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wake kuwa kuanzia sasa mwandishi anatakiwa kulipwa Sh. 60,000 kwa kazi atakayofanya na kwa siku iwapo atalala anatakiwa kulipwa Sh.120, 000.

Mtanda akasisitiza hafurahishwi kuona mwandishi wa habari analipwa Sh. 30,000 kwa kazi anayofanya. Naomba nikupongeze Mkuu wa Mkoa wa Mara,  Said Mtanda.Umedhihirisha upendo wako mkubwa kwa wanahabari wa Tanzania, unaweza kuona kauli hiyo ni kwa waandishi wa Mara pekee.

Kwangu naitazama kauli hiyo kama ukombozi kwa waandishi wa maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Sio mara tu hata Dar es Salaam,  Dodoma,  Mwanza, Shinyanga, Mtwara, Ruvuma, Kilimanjaro,  Arusha,  Kigoma.

Yaani kauli ya Mtanda inakwenda mbali zaidi hadi Rukwa, manyara, Singida,  Pwani, Morogoro, ndio inakwenda mbali,  kwa lugha rahisi ni kauli inayoleta faraja kwa waandishi wa mikoa yote. Nikiri Mtanda alikuwa akizungumza katika mkoa wake,  lakini jambo zuri sio vibaya likitekelezwa na mikoa mingine.

Kuna ubaya gani alichokisema Mkuu wa Mkoa Said Mtanda kikiigwa na kutekelezwa na Mkuu wangu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila?

Kuna ubaya gani alichokisema Mtanda kikatekelezwa na dada yangu Fatma Mwasa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera,  dada aliyesaidia kuanzisha safari yangu ya uandishi akiwa Mhariri Mkuu wa Gazeti la Mwanamke ambalo lilikuwa chini ya Kampuni ya Bussines Times.

Ni kitambo sana na hiyo itakuwa na siku yake na hapo kuna wengine walinishika mkono. Kuna msemo unaosema ukimuona kobe yuko juu kuna aliyempandisha. Niko niliko kwa sababu wapo walionishika mkono.

Lakini nauliza tena kuna ubaya gani alichokisema Mtanda kikitekelezwa na kaka yangu Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaj Aboubakari Kunenge? Kuna ubaya gani? Nauliza na kuwaza tu.

Hivi alichokisema kuhusu waandishi wa habari na malipo yao kuna dhambi gani kikifuatwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya rafiki yangu Juma Homela ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Najaribu  kuuliza kuna ubaya gani alichokisema Mtanda kikiigwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas?

Najaribu kuuliza hivi kuna ubaya gani alichokisema Mtanda kikaigwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma dada yangu Rosemary Senyamule? Huenda nawaza vibaya lakini tufanye hivi tuwaze wote. Tuwaze alichosema Mkuu wa Mkoa wa Mara Mtanda kuhusu posho kwa waandishi wa habari.

Kuna ubaya gani hiki alichokisema Mtanda kikaigwa na baba yangu Makongoro Nyerere ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Wakati tunaendelea kuwaza kauli ya Mtanda naomba kurudia tena kumpongeza kwa kutambua hadhi ya Mkuu wa Mkoa lakini kuona na kuthamini kinachofanywa na waandishi wa habari nchini.

Kwanza sio siri waandishi  wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu. Hakuna anayewasemea wala kuwapigania. Wanatumiwa sana lakini wanadharauliwa sana. Nitatoa mifano ipo huko chini.

Kwanza soma ninachoandika kuhusu Mtanda. Binafsi amenikosha,  amenifurahisha na kwangu kauli yake kuhusu waandishi inakuwa moja ya kauli bora ambazo zimetolewa na wakuu wa mikoa kwa mwaka 2023.

Ngoja nieleze kitu kuhusu waandishi wa habari, na niseme tu katika eneo hili la habari sina muda mrefu lakini nilianza mwaka 2001 nikiwa gazeti la Majira, gazeti lililokuwa likiongozwa kwa kusomwa na Watanzania.

Majira ndilo lilikuwa gazeti kinara kwa miaka mingi huko nyuma,  baadaye magazeti mengine yakachukua nafasi. Ndivyo hivyo.

Basi huko ndiko nilianza kuandika, na kubahatika kulitumikia. Majira kuanzia mwaka 2001 mpaka mwaka 2009 nilipojiunga na gazeti jipya la Jambo Leo ambalo nikiri lilinifanya nijidai, niringe, nitambe.

Nakushukuru Juma Pinto na rafiki yako Ben Kisaka kwa kuanzisha Jambo Leo na mimi kuwa mmoja wa waandishi watano wa mwanzo tulioanza safari ya gazeti hilo. Nilikuwa na akina nani nao huu ni mjadala wa siku nyingine.

Hivyo ninapozungumzia waandishi wa habari na maisha yao naweza kuwa na nafasi ya kusema japo kidogo maana najua kuna manguli wa habari wengi tu na wanajua maisha yetu. Kwa lugha rahisi niko katika uandishi wa habari kwa mwaka wa 22 kama sio 23.

Na kwa sasa niko na Michuzi Media Group inayomiliki Michuzi Blog na Michuzi TV. Ahsante kaka na baba yangu Muhidin Issa Michuzi maarufu kwa jina la Ankali kwa kuanzisha kampuni hii miaka mingi iliyopita. Tunaishi kupitia Michuzi Blog na Michuzi TV na maisha yanasonga. Anayedharau na adharau lakini kwa Michuzi kuna Michuzi.

Nimetoa sehemu ya historia yangu kidogo nikiwa na lengo moja tu la kuungana na Mkuu wa Mkoa Said Mtanda, kauli yake imegusa eneo ambalo kwangu ndio maisha yangu. Ndio ugali wangu ulipo. Akitokea kiongozi akatoa neno la faraja siwezi kukaa kimya, lazima nipongeze na nakupongeza Mtanda.

Ukweli wapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakitambua mchango wa waandishi wa habari, viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi na waandishi na kuwalipa posho nzuri tu.

Lakini hakuna allyewahi kutamka hadharani kama Mtanda kuhusu posho kwa waandishi. Ni kweli uandishi wa habari ni huduma isiyo na malipo, lakini katika mazingira ya sasa kuna ubaya gani kiongozi wa umma ukimwita mwandishi wa habari ukamlipa na posho inayoeleweka. Mpe posho nzuri afanye kazi yako vizuri.

Kuna baadhi ya wakuu wa mikoa wao kazi yao ni kuwatumikisha tu waandishi wa habari kutwa nzima, asubuhi hadi jioni halafu wakati wa kuagana analipa Sh. 20, 000 au Sh. 25, 000 na hapo sura kaikunja utadhani kakanyaga mwiba wa mbigili. Acheni bwana.

Na hao ndio ambao ukifika muda wa taarifa ya habari wanakaa kusubiri habari yake itoke na isipotoka simu kibao. Nadhani umefika wakati pia kwa maofisa habari sio tu katika ofisi za wakuu wa mikoa, lakini katika ofisi zote za umma mnapoweka bajeti zenu kwa waandishi fikirieni na viwango.

Wakati mwingine shida haiko kwa Mkuu wa Mkoa bali iko kwa wakuu wa idara na vitengo vya habari na mawasiliano. Linapofika suala la posho za waandishi wanaona kama vile hawastahili kulipwa wakati wenyewe wanalipwa mshahara na posho wanachukua, lakini posho kwa waandishi wanaona hastahili.

Ukweli kuna baadhi ya maofisa habari wamekuwa wakiwachukia waandishi wa habari, na hakuna sababu ya maana, zaidi ya posho tu. Wengine wamekuwa na kazi ya kuwaandikisha majina katika karatasi za malipo na wala hakuna wanacholipa. Hovyo kabisa.

Kauli ya posho ya waandishi wa habari ya Sh. 60,000 hadi Sh. 120,000 uwe mwanzo mpya kwa maofisa habari wa mikoa, wilaya na taasisi nyingine kuanza kujipanga na mkiamua mnaweza. Taasisi binafsi na mashirika binafsi wala hawana tatizo, viwango vyao vya malipo ya posho kwa waandishi wa habari vimejitosheleza haswaa, ukiitwa unasema hapa kuna maisha.

Lakini niwe mkweli yapo baadhi ya mashirika na taasisi za Umma Mashallah wanalipa vizuri, tena wanalipa vizuri sana. Hao sina tatizo nao zaidi ya kuwapongeza. Sitaki kuchuma dhambi wanaishi na waandishi vizuri. Nawashukuru kwa niaba ya wenzangu.

Hata hivyo, nikiri katika hili la kupigania maslahi ya waandishi wa habari hata waandishi wenyewe kwa wenyewe kuna wakati wanawekeana kauzibe. Wakubwa zetu wako kimya. Wametengeneza miraja yao wamepiga kimya. Wanabunya tu wala hawawafikirii waandishi walio wengi. Sijui wakoje? Nakushukuru kaka yangu Mtanda kwa kupaza sauti kuhusu waandishi wa habari.

Pamoja na yote hayo uliyoyasoma hapo juu naomba hili uliweke akilini mwako, ni hivi namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye baada ya kuona changamoto zinazowakabili waandishi wa habari aliamua kumwagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,  Nape Nnauye kuunda Tume kufuatilia hali ya uchumi kwa vyombo vya habari.

Waziri Nape alimteua Mzee wetu Tido Mhando kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo yenye wajumbe kadhaa akiwemo kaka na shemeji yangu Richard Mwaikenda. Ni matumaini yangu tume hiyo itakuja na majibu na bahati nzuri nina imani kubwa na kaka Nape, anawapenda waandishi wa habari na sisi tunampenda. Kwa leo inatosha.

Alamsiki.

0713833822

Share To:

Post A Comment: