Na Mwandishi wetu, Karatu Arusha.
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inaendeleea na zoezi la kuhamisha wenyeji waishio ndani Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiyari ambapo leo tarehe 12 Januari, 2024 Jumla ya kaya 44 zenye watu 296 na mifugo 1,206 zimeagwa rasmi.
Wakati akiwaaga wananchi hao katika ofisi za NCAA Karatu Mkoani Arusha, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Richard R. Kiiza amewaomba wananchi waliondoka leo kuwa mabalozi na kuwaelimisha wale ambao bado hawajiandikisha kuona faida za kuhama ili waweze kupata nafasi ya kutumia fursa hii kujiendeleza na kuwa na maisha bora.
"Wenzenu waliokwisha hamia Msomera na maeneo mengine wanaendelea kupata maisha bora kutokana na kujengewa na kuboreshewa huduma zote muhimu za Kijamii na walio wengi wameshaanza shughuli za Kilimo na wanategemea kupata chakula cha kutosha" ameongeza Kiiza.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo Kamishna Msaidizi Mwandamizi Fedes Mdala ambaye ni Meneja wa mradi huo amesema kuwa hadi kufikia leo tarehe 12/01/2024 jumla ya kaya 1,069 zimejiandikisha kuhama kwa hiyari ndani ya Hifadhi ambapo kati ya kaya hizo kaya 633 zenye watu 3,526 na mifugo 16, 896 zimeshahama kutoka ndani ya hifadhi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wanaohama Bw. Wilfred Makamero ameeleza sababu zilizomfanya akubali kuhama kwa hiyari na kusema “Naishukuru Serikali kwa kutupatia huduma zote za maendeleo kwa kipindi chote ambako tumeishi hifadhini mpaka sasa tunapoamua kuhama kwa hiyari yetu kuelekea Msomera ili tukapate fursa ya kujiendeleza wenyewe tofauti na tulivyokuwa hifadhi kwani shughuli za kimaendeleo kama kulima haziruhusiwi” amesema Bw. Makamero.
Kwa upande wake Bibi Inoti Moses aliongezea kwa kumshukuru Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fursa ambayo wameahidi kuitumia vizuri ili kupata maendeleo na kuziendeleza familia zao.
Zoezi hili la kuhamisha wenyeji wanaoshi ndani ya Hifadhi kwa hiyari ni endelevu ambapo zoezi la uandikishaji linaendelea na wanapewa fursa ya kuchagua mahali popote wanapotaka kwenda au kwenda kwenye maeneo yaliyotengwa na serikali Msomera Wilaya ya Handeni, Kitwai Wilaya ya Simanjiro na Saunyi Wilaya ya Kilindi.
Post A Comment: