WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wasikubali kutoa rushwa mahali popote huku akisisitiza kuwa wananchi ni wadau muhimu sana katika mapambano dhidi ya vita hiyo.

“Ninyi ni wadau wakubwa wa kukomesha rushwa. Nyie ni wadau wakubwa wa kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Ili nchi yetu isiwe na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, wananchi mnapaswa kufichua vitendo vya ukosefu wa maadili na uvunjifu wa haki za binadamu,” amesema.

“Mtanzania usikubali kutoa rushwa popote, hasa kwenye maeneo unayopaswa kupewa huduma hiyo. Wewe ni Mtanzania unalindwa na sheria za nchi za kupata huduma bure kama vile hospitali bila kutoa rushwa. Inatakiwa kila Mtanzania abebe jukumu hili kwa mikono miwili, alisimamie na alitekeleze,” amesisitiza.

Ametoa wito huo leo (Jumapili, Desemba 10, 2023) wakati akizungumza na washiriki na wadau mbalimbali kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika Nyerere Square, jijini Dodoma.



Waziri Mkuu ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Mheshimiwa Rais amesisitiza umuhimu wa kila mmoja kuendelea kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na vitendo vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo:“Zingatia Maadili, Utu, Uhuru na Haki kwa Maendeleo Endelevu.”


Waziri Mkuu amesema kaulimbiu hiyo inachagiza masuala ya msingi yanayohusu maendeleo endelevu kutokana na ukweli kwamba kizazi huru chenye uadilifu, utu na kinazingatia haki ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote.


“Hivyo basi, hatuna budi wananchi wote kuunganisha nguvu katika ujenzi wa kizazi chenye misingi ya maadili. Kaulimbiu hii ni wito kwa sekta ya umma na sekta binafsi kutimiza wajibu wake kuhusu masuala ya maadili, utu, uhuru na haki. Kwa maneno mengine kaulimbiu hii imegusa taasisi zote na inasisitiza uwajibikaji wa kila mmoja wetu.”

Akisisitiza umuhimu wa maadili wa jamii, Waziri Mkuu amesema: “Maadili yanajengwa kuanzia kwenye taasisi ya kwanza ambayo ni familia. Taasisi ya pili ni shule, ambayo inawajibika kuweka mifumo ya kuendeleza kile kilichopatikana nyumbani. Kadhalika nyumba za ibada, tunategemea ziwe chachu ya kujenga maadili mema kwa misingi ya kiroho na hatimaye ushiriki wa jamii nzima kupitia wazee wa ukoo, jadi na maarufu katika makuzi ya mtoto.”

Waziri Mkuu pia alizindua Awamu ya Nne ya Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na kuugawa nakala kwa wadau na baadhi ya wawakilishi wa makundi yaliyokuwepo.

Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Simbachawene alisema maadhimisho hayo kimataifa huwa yanafanyika Desemba 9, kila mwaka lakini hapa nchini yanafanyika Desemba 10, kwa sababu ya kupisha maadhimisho ya siku ya Uhuru. “Haya ni maadhimisho ya nane kufanyika kitaifa, tangu tuanze 
mwaka 2016,” alisema.


Alisema katika kuhakikisha haki za raia zinalindwa nchini, Rais Dkt. Samia aliunda Tume ya Haki Jinai ili ipate maoni ya wananchi na wadau mbalimbali yatakayofanyiwa kazi ikiwa ni dhamira yake ya kulinda haki za watu wote.





Share To:

Post A Comment: