Waumini wa Kigango cha Roho Mtakatifu Parokia ya Watakatifu Wote ya Nzuguni Jijini Dodoma wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde kwa kusaidia kukamilisha ujenzi wa kanisa la kigango kwa kuezeka kanisa lote ambalo hapo awali waumini walikuwa wanaabudu huku jua na mvua zikileta changamoto kubwa.
Paroko wa Parokia ya Watakatifu wote Nzuguni Fr. Joseph Kazikunema aliongoza Ibada hiyo ya shukrani na kutumia fursa hiyo kumshukuru Mbunge Mavunde kwa niaba ya waumini wote kwa namna ambavyo amekuwa akijitolea katika kazi za kanisa na kumuombea baraka kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumjaalia moyo wa kujitoa.
Akizungumza katika Ibada hiyo Anthony Mavunde ambaye pia aliongozana na Diwani wa Kata ya Nzuguni Mh. Alloyce Luhega amesema anamshukuru Mungu kwa kumjaalia kutoa sadaka ya ujenzi wa kanisa kwa kuchangia mabati yenye thamani ya Tsh 9,000,000/= na hivyo kuwezesha waumini hao kushiriki ibada katika mazingira rafiki.
Mbunge Mavunde pia alitoa mchango wa Kinanda chenye thamani ya Tsh 5,000,000/= kwa ajili ya Kwaya ya Kigango cha Roho Mtakatifu.
Akitoa maelezo ya awali Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Walei wa Kigango cha Roho Mtakatifu Ndg. Isaya Ntalugela amesema ujenzi wa kanisa hilo lilianza kwa nguvu za waumini kuchangia ujenzi wake ambapo kazi kubwa ilibaki ni ya kupaua,na hivyo kumshukuru Mbunge Mavunde kwa kusaidia kukamilika kwa ujenzi huo.
Post A Comment: