Na Munir Shemwera, WANMM MOROGORO
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda amesema Wananchi wa Ngorongoro wanaohamishwa kutoka eneo la hifadhi kwenda kijiji cha Msomera Handeni mkoa wa Tanga wamehamishwa kwa kuzingatia haki za binadamu.
Mhe. Pinda amesema hayo tarehe 4 Desemba 2023 mkoani Morogoro wakati akifungua kongamano la siku mbili linaloratibiwa na Jukwaa la Ardhi Tanzania (TALA) kujadili masuala ya ardhi.
Amesema, pamoja na uwepo wa taasisi zenye mapenzi mema na serikali lakini zipo baadhi yake za binafsi zinazofanya biashara kwa kuuza nafsi za watanzania wanaoishi Ngorongoro kwa kuwarubini na kuelezea maneno yasiyokuwa na uhalisia kuhusu kuhamishwa kwa wananchi wanaoishi kwenye hifadhi hiyo.
Amelitaka Jukwaa la Ardhi Tanzania (TALA) na wadau wa mkutano huo kwenda kijiji cha Msomera mkoani Tanga na watakapotoka huko serikali iko tayari kupokea maoni kwa kuwa wao ni watanzania na wanawasemea watanzania wenzao.
Akigeukia suala la haki za binadamu, Naibu Waziri Pinda amesema ni haki gani anazozikosa mwananchi anayeishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na kwanini asitafutiwe haki hiyo? Ameweka wazi kuwa, Seikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya jitihada kuhakikisha inawajengea uwezo wale waliohamishiwa kijiji cha Msomera.
‘’Leo wananchi hao wanaweza kwenda benki wakakopoa, wana ardhi ya kudumu na hati, hakuna mtu atakayewabughudhi, kuwanyang’anya na wametengewa maeneo makubwa ya kuchungia mifugo yao na tunaendelea kuboresha na tunachimba mabwawa kuhakikisha wananchi hawatupwi na wanalindwa na mali zao’’ alisema Pinda.
Amesema, Ngorongoro kwa mujibu wa Sheria ilikuwa siyo rahisi kupeleka huduma nyinginezo kwa sababu sheria inayolinda eneo hilo ilikuwa ni sheria iliyotaka kutoharibiwa Ecolojia ya Ngorongoro.
Naibu Waziri Pinda amewaambia washiriki wa kongamano hilo kuwa si vizuri kupotoshana katika suala la Ngorongoro na kueleza kuwa, pale inapopatikana nafasi ya kujadili basi yajadiliwe matokeo halisi ya kitaifa na kusisitiza kuwa ni lazima kujengeana ubora kwa maisha ya watanzania.
Kongamano hilo la siku mbili lililobeba kauli mbiu ya Usalama wa Milki za Ardhi kwa Uhakika wa Chakula limejadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya ardhi ikiwemo Haki za Wanawake katika Muktadha wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi na Usalama wa Chakula, Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Uratibu wa Takwimu pamoja na Hali ya Haki za Ardhi kwa Vijana na Utekelezaji ya Mikakati na Uhamasishaji Vijana Kushiriki katika Kilimo.
Post A Comment: