WANANCHI wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wameendelea kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa saratani mbalimbali ikiwemo ya mlango wa kizazi na matiti kwa wanawake pamoja na saratani ya tezi dume kwa wanaume.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 12, Dk. Maguha Stephano, Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma, amewasisisitiza wananchi wIlayani humo kuchangamkia fursa hiyo na kufika Kituo cha Afya Kabuku kupata huduma hiyo.

Ameeleza huduma hiyo inatolewa bila malipo, hivyo ni fursa kwa kila mwananchi kukitokeza atambue hali ya afya yake kwa upande wa saratani ili kuwawezesha kuanza matibabu watakaogundulika kuwa na tatizo hilo.

Pia, amesisitiza walengwa wa huduma hiyo ni wananchi wote wenye dalili na wasio na dalili za magonjwa.

Dk. Stephano amewasihi wanaume kufika na kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya tezi dume unaofanyika kwa kutumia kipimo cha damu kama inavyofanyika kwa ugonjwa wa malaria.

Huduma hiyo inatolewa kupitia kampeni ya elimu na uchunguzi wa saratani inayotolewa Desemba 10 hadi 16, mwaka huu.

Ratiba ya kampeni hiyo inaonyesha kuwa Desemba 10 na 11 itatolewa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni,Mkata, Desemba 12 na 13 itatolewa katika Kituo cha Afya Kabuku.

Aidha, Desemba 14 itatolewa katika Kituo cha Afya Kideleko, Desemba 15 na 16 itatolewa katika Hospitali ya Wilaya Handeni Mjini.

Kampeni hiyo inafanyilka kwa udhamini wa Benki ya NBC.

Share To:

Post A Comment: