NAIBU  Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akiwa ameongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Afya mapema leo Desemba 4, 2023  wamewasili Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kuona hali ya utoaji huduma na kutoa pole kwa majeruhi 11 wa maafa ya mafuriko yaliyotokea katika mji wa Katesh Wilaya ya Hanang Mkoa wa Manyara ambao wamelazwa katika Hospitali hiyo.

Akizungumza akiwa katika hospitali hiyo leo Desemba 4, 2023, Dkt. Mollel amesema kuwa Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha wanatoa huduma bora za matibabu ili kuokoa maisha ya watu, amesema kuwa hadi sasa Hospitali zote ndani ya Mkoa wa Manyara zimepokea na kuhudumia majeruhi 93 na wote wanaendelea vyema na matibabu.

Amesema Wizara ya Afya imeratibu upatikanaji wa timu za Madaktari kwa ajili ya kuongezea nguvu katika Hospitali za Mkoa wa Manyara ili kuweza kutoa huduma bora na kwa haraka zaidi kwa majeruhi ambapo amebainisha kuwa madaktari hao wametoka katika Mikoa ya Arusha, Dodoma na Singida.

“Huduma zinatolewa vizuri, hakuna kilichokosekana na wagonjwa wanaendela vyema na matibabu, kila kitu kinaenda vizuri kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza jana, "amesema Dkt. Mollel.

Mapema leo asubuhi Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sengida amesema kuwa idadi ya vifo vya watu waliofariki dunia kutokana na mafuriko yaliyotokea imeongezeka kutoka watu 47 hadi kufikia 49 baada ya kupatikana kwa miili mingine miwili.

Hapo baadae Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kufika katika Mkoa wa Manyara kujionea hali ya maafa, kutembelea na kutoa pole kwa majeruhi pamoja na kufanya kikao na watendaji katika kushughulikia maafa ya Katesh.











Share To:

Post A Comment: