Afisa Mtafiti wa Soko la Ajira Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati , Sadan Komungoma akizungumza wakati akifungua mafunzo ya ufugaji bora wa mbuzi na kondoo yaliyofanyika hivi karibuni Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Kulia ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka VETA Mkoa wa Singida, Dkt. Dickson Mkopi na kushoto ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo Afisa Mifugo Wilaya ya Bahi, Daniel Kilogo.
...................................................
Na Dotto Mwaibale, Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati imeendelea
kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanainuka kiuchumi kupitia sekta
mbalimbali ikiwemo ya ufugaji kwa kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa mbuzi na
kondoo kwa wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Mafunzo hayo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo katika wilaya hiyo yamelenga
kuwawezesha wafugaji kuondokana na ufugaji wa mazoea kwenda kwenye ufugaji wenye
tija utakaowakwamua kiuchumi.
Afisa Mtafiti wa Soko la Ajira VETA Kanda ya Kati, Sadan Komungoma akizungumza
wakati akifungua mafunzo hayo hivi karibuni alisema VETA Kanda ya Kati ambayo
inahusisha Mikoa ya Manyara, Dodoma na Singida wamekuwa wakifanya utafiti wa
kuangalia shughuli za kiuchumi zinazofanyika kwenye maeneo husika ambapo
kupitia utafiti huo wilayani humo waligundua pamoja na shughuli nyingi
zinazofanyika upo pia ufugaji wa wanyama wa aina tofauti tofauti.
Alisema utafiti huo uligundua kuwa wananchi wa wilaya hiyo licha ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi wanajishughulisha pia na ufugaji wa
mbuzi, kuku, ng’ombe na kondoo lakini wanapofuga hutumia eneo kubwa huku kukiwa na uharibifu
mkubwa wa mazingira.
“Katika utafiti wetu tuligundua kuwa nchi inakuwa na maeneo mengi yamekuwa
yakitumika kwa shughuli mbalimbali za uzalisha hivyo tukaona kuna haja sasa ya
kuja na mafunzo ya kuwawezesha wafugaji ili waweze kufanya ufugaji mkubwa
lakini katika eneo dogo,” alisema Komungoma.
Alisema kufuatia utafiti huo walioufanya Mkoa wa Dodoma hususan Wilaya ya
Bahi walibaini kuwepo kwa wafugaji wengi ambao wanafuga lakini ufugaji wao hauna tija unakuta mtu anamifugo kidogo lakini anatumia eneo kubwa na kuleta
changamoto kwa watu wengine ikiwa ni pamoja na mifugo yao kuingia kwenye mashamba ya
wakulima na kula mazao yao.
Alisema baada ya utafiti huo wakaona wawapekee mafunzo hayo ambayo
yatawafanya watumie eneo dogo kwa ufugaji wa mifugo mingi jambo ambalo
litaisaidia Serikali kufanya shughuli zingine za maendeleo katika eneo ambalo
lingetumiwa na wafugaji wachache kama malisho ya mifugo.
“Mafunzo haya ambayo yamewahusisha wafugaji zaidi ya 58 tunaimani yataisaidia jamii
na wafugaji wa wilaya hii ya Bahi kufanya ufugaji bora na wenye tija kwa
kutumia eneo dogo na kuwa mabalozi kwa wananchi wengine jambo litakaloisaidia halmashauri ya wilaya katika utunzaji wa ardhi ambayo ingetumika kwa kundi moja
tu la wafugaji,” alisema Komungoma.
Washiriki wa mafunzo hayo, Celina Mbete, Julius Chimwela, Stephano Petro na
Mwadawa Mhando waliishukuru Serikali kupitia VETA kwa kuwapelekea mafunzo hayo
ambayo yamewabadilisha kwa kuacha ufugaji wa kimazoea na kwenda kufanya ufugaji
wenye tija.
“Kutokana na mafunzo haya naenda sasa kufanya ufugaji wa kibiashara ambapo nitaanza na uzalishaji wa mbuzi 20 hadi kufikisha mbuzi 244 baada ya miaka
mitatu,” alisema mfugaji Julius Chimwela.
Mfugaji Celina Mbete alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya mafunzo ambapo alitumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa VETA Kanda ya Kati
chini ya Mkurugenzi wake John Mwanja na watendaji wenzake kwa kuwapa kipaumbele
wafugaji wa Wilaya ya Bahi kupata mafunzo hayo.
“Binafsi nakosa cha kusema zaidi ya kumshukuru Rais wetu Mama Samia kwa
kutuletea fedha hizi pia nitakuwa mchoyo wa fadhira kama sitaupongeza uongozi
mzima wa VETA kwa kufanya utafiti wao na kubaini uhitaji wetu wa mafunzo haya
ambayo yatatusaidia kufanya ufugaji wa wanyama kwenye eneo dogo,”
alisema Mbete.
Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Chuo cha VETA Wilaya ya Bahi, Daudi Lyanga
aliishukuru Serikali kwa kupeleka mafunzo hayo ambayo ni muhimu kwa jamii ya
wafugaji ambapo alitumia nafasi hiyo kutangaza kozi mbalimbali zitakazoanza
kutolewa katika chuo hicho kuanzia Januari 2024.
Lyanga alisema katika chuo hicho kuna kozi za muda mfupi ambazo ni ufundi
wa magari, kozi ya kompyuta, ushonaji nguo, umeme wa majumbani, ufundi washi,ufundi
bomba, ufundi wa kuunganisha vyuma, udereva wa bajaji na pikipiki, udereva wa
awali na ujasiriamali ufugaji na kilimo.
Alisema kwa kozi za muda mrefu zitakazotolewa zitakuwa ni ya ufundi washi
na kuunganisha vyuma na akawaomba vijana wa wilaya hiyo kwenda kuomba nafasi ya
kuanza kozi hizo ambazo gharama yake ni ndogo.
Lyanga alisema kuwa kwa gharama za kozi hizo na namna ya kuomba nafasi hizo unaweza kuwasiliana na ofisi ya msajili wa chuo hicho kwa namba 0769-895643 au namba 0786-281937 au mwombaji kufika Chuo cha VETA Wilaya ya Bahi.
Post A Comment: