NA DENIS CHAMBI, TANGA.
TAASISI ya Umoja wa amani Kwanza imempongeza Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha, kusimamia na kuboresha misingi ya amani kwa Taifa ambayo imekuwa ni kielelezo kwa mataifa mbalimbali hususani ndani ya Africa.
Pongezi hizo wamezitoa leo December 16 mkoani Tanga katika hafla iliyoambatana na kumpongeza rais wa taasisi hiyo Dkt Wilson Munguza kwa kutunukiwa cheo cha udaktari na rais wa amani kwanza Afrika Mashariki iliyotolewa hivi karibuni na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Akimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Tanga katika hafla hiyo , Mkurugenzi wa Halmashauri jiji la Tanga Said Majaliwa ameipongeza taasisi hiyo kwa jitihada inazozifanya kwa kuvisaidia vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kutekeleza na kusimamia majukumu yake ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa amani kwa Taifa ambayo huchochoea maendeleo kupitia nyanja mbalimbali.
Majaliwa amesema taasisi hiyo isiyokuwa ya kiserikali itaendelea kupata ushirikiano wa hali na mali kutoka serikalini katika kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuilinda amani kwa Taifa ambayo imekuwa ikiwavutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.
Awali akizungumza rais wa Umoja wa amani kwanza Dkt Wilson Munguza amesema wataendelea kuwa msaada kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha amani inakuwepo na katika kuhakikisha wanawafikia watanzania wote wana malengo ya kufika hadi ngazi ya kata ili kutoa elimu na kusisitiza uzalendo kwa Taifa.
Aidha Dkt. Munguza ameiomba Serikali kuwashika mkono katika kutimiza lengo lao la kujenga chuo cha amani katika wilaya ya Handeni mkoani Tanga kinachotarajiwa kuchukua wanafunzi kutoka ndani na nje ya Afrika mashariki.
" Ombi la taasisi kwa serikali ya mkoa wa Tanga tunaomba kuelekea lengo letu la kujenga chuo cha Amani katika wilaya ya Handeni tunaomba kupelekewa Buldoza litakalosaidia kusafisha eneo ambalo tunatarajia kujenga chuo hicho ambacho kitachukua wanafunzi wa kutoka ndani ya Nchi za Afrika Mashariki" alisema Dkt Munguza .
Akitoa salamu za jeshi la polisi kwa niaba ya kamanda wa mkoa wa Tanga , mkuu wa kitengo cha Polisi jamii kamshina msaidizi wa Polis ACP Yohana Mjengi ameipongeza taasisi hiyo kwa kazi wanazoendelea kuzifanya wakishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha amani inaendelea kuwepo.
Aidha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kuwa mabalozi wa amani katika kuwavumbua wahalifu sambamba na kuwataka madereva na wanatumia vyombo vya usafiri kuzingatia usalama barabarani ili kuepukana na matukio ya ajali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu na mali zao.
"Tumetika ofisini kwenda mpaka kwenye vijiji vitongoji na hata mitaa kwaajili ya kuongeza ulinzi shirikishi niwapongeze sana umoja wa amani kwanza kwa kutambua umuhimu wa amani sisi Polisi na wao majukumu yetu yanafanana tumekuwa tukishirikiana nao mara kwa mara katik kutoa elimu ya kuimarisha amani maendeleo yeyote pasipo kuwa na amani hayawezi kuja" alisema ACP Mjengi.
"Jeshi la Polisi linawataka wananchi wote kuimarisha ulinzi na usalama hasa katika kipindi hiki kuelekea mwisho wa mwaka kuhakikisha tunakuwa mabalozi wa amani na kwa upande wa madwreva kuzingatia sheria za usalama barabarani , wananchi wachukue tahadhari za kiusalama hasa tunapokuwa kwenye mikusanyiko" alisisitiza.
Taasisi hiyo ya Amani Kwanza ambayo ilianzishwa mwaka 2018 ikiwa na wanachama 14 inaendelea kukua ambapo sasa imeweza kufikisha zaidi ya wanachama 5, 000 ikiwa ipo katika mikoa yote ya Tanzania.
rais wa Umoja wa amani kwanza Tanzania Dkt Wilson Munguza akizungumza katika hafla hiyo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Tanga Said Majaliwa akimwakilisha mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba katika hafla ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika leo December 16,2023 katika Hotel ya Panoli jijini Tanga ikiwa imeandaliwa na Umoja wa Amin kwanza.
Mkuu wa kitengo cha Polis jamii mkoa wa Tanga ACP Yohana Mjengi akizungumza katika hafla hiyo ikiwa amemwakilisha kamanda wa Jeshi la Polis mkoa wa Tanga.
Post A Comment: