Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

 

Serikali inaendelea kusimamia ufuatiliaji wa tathmini katika utekelezaji wa majukumu ya Sekta ya Ardhi na uadilifu katika utoaji wa huduma za Ardhi nchini.

 

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda tarehe Desemba 2023 mkoani Morogoro wakati akifungua kongamano la masuala ya Ardhi nchini.

 

Amesema, hatua muhimu za kinidhamu na ufuatiliaji zilizochukuliwa na wizara yake ni pamoja na kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi tija na uwazi katika utoaji wa huduma.

 

Kwa mujibu wa Mhe Pinda, hatua nyingine ni kusimamia uadilifu kupitia vikao vya Kamati za Kudhibiti Uadilifu ili kujadili na kuishauri Wizara kuhusu masuala ya uadilifu katika utendaji kazi, kwa kupitia kamati za nidhamu.

 

‘’Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imewachukulia hatua za kinidhamu watumishi wanaokiuka maadaili ya kazi ambapo 12 wamefukuzwa kazi, watumishi nane (8) wameshushwa ngazi ya mishahara, watumishi wawili (2) wamepewa onyo na watumishi watano (5) wameshushwa vyeo lengo la hatua hizo ni kuongeza ufanisi katika kazi na kulinda haki za wananchi’’. Alisema Mhe. Pinda

 

Hata hivyo, Naibu Waziri Pinda aliwaambia washiriki wa kongamano hilo la siku mbili lililobeba ujembe wa Usalama wa Milki za Ardhi kwa Uhakika wa Chakula kuwa, serikali itahakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi za umiliki wa ardhi na makazi.


‘’Tunafahamu Watanzania walio wengi na ambao ni maskini wanaishi vijijini na Wizara ina dhamana ya kusimamia eneo hili, kama Wizara tutajitahidi kwa kadri na uwezo wetu na kuendelea kushirikiana na wadau wetu na Wananchi wote kuhakikisha nyaraka rasmi za umiliki ardhi na makazi zinatolewa na kuendelea kukabiliana na changamoto zilizopo nchini kuhusu migogoro ya ardhi’’. Alisema Pinda.


Amewaomba wananchi kuendelea kutii Sheria na taratibu zilizowekwa za umiliki wa ardhi na makazi na kuahidi kuwa taarifa itakayotokana na majadiliano ya kongamano hilo wataifanyia kazi.

 

Awali Mratibu wa Kogamano hilo lililoandaliwa na Jukwaa la Ardhi Tanzania (TALA) Benard Baha amesema Jukwaa la Ardhi Tanzania ni jukwaa linaundwa na wanachama wanaowakilisha makundi mbalimbali ya kijamii kama vile wakulima, vijana pamoja na wafugaji wanaotegemea zaidi ardhi katika kuendesha maisha yao.


Amewataja baadhi ya wanachama hao kuwa ni pamoja na HAKIARDHI, Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania, Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

 

‘’Jukwaa pia ni mwenyeji wa mashirika wanachama wa Jukwaa la Ardhi la Kimataifa linalojumuisha taasisi za ndani na za kimataifa zinazofanya kazi zake nchini  ambapo TALA imepewa jukumu la kuratibu utendaji kazi wa taasissi hizo kwa namna inavyoshirikisha jamii’’. Alisema Baha

Mratibu huyo wa Jukwaa la Ardhi Tanzania amefafanua kuwa, kumekuwa na utatamaduni wa kukutanisha wadau kujadili na kutafakari masuala mbalimbali kuhusu milki na utawala wa ardhi pamoja na tathmini katika masuala ya sekta ya ardhi utamaduni alioueleza kuwa, unatoa mwanya wa kusikiliza taarifa za kitafiti, maelezo na ushuhuda kutoka kwa wananchi suala lilalotoa fursa kwa jukwaa hilo kutoa mapendekezo kwa serikali juu ya maeneo yanayohitaji maboresho.

 

Share To:

Post A Comment: