Na John Walter-Manyara
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, amekusanya kiasi cha tani 78.5 za mbolea zenye thamani ya shilingi Milioni 129,449,094 kutoka kwa wadau wa mbolea zitakazokabidhiwa kwa waathirika wa mafuriko ya tope yaliyotokea Wilayani Hanang katika mji mdogo wa Katesh hivi karibuni.
Laurent amekabidhiwa kiasi cha tani 65 za mbolea za kupandia na kukuzia leo tarehe 7 Desemba, 2023 zilizotolewa na wazalishaji na wafanyabiasha wa mbolea nchini.
Amepokea tani 30 za mbolea kutoka kampuni la Mbolea la Taifa (TFC), tani 30 kutoka Kampuni ya Uzalishaji wa Mbolea Itracom na kiasi cha tani 5 kutoka Kampuni la Mbolea na Uchimbaji madini Minjingu.
Aidha, Laurent ameeleza kuwa, anataraija kupokea mbolea za misaada kutoka kampuni la mbolea la Staco tani 10, Yara tani 2.5 na tani 1 kutoka kampuni la mbolea la Premium.
Amesema, milango iko wazi kwa wadau wa mbolea kufikisha misaada yao itakayowasaidia waathirika wa mafuriko wakati huu wa msimu wa kilimo kutokana na kuwa wakulima walikuwa wamenunua mbolea ambazo hazijazaa matunda kutokana na athari za mafuriko walizokutana nazo.
Akizungumzia hali ya usajili kwenye mfumo wa mbolea za ruzuku, Laurent amesema, wakulima 8449 wa Hanang wamejiandikisha na walishanunua kiasi cha tani 1131.2 za mbolea mpaka wanapopata majanga haya.
Post A Comment: