Naibu waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde amekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kuja na mpango wa kuanzisha mitaala itakayohusu masuala ya Kilimo-biashara, Ufugaji, Ufundi na utalii zitakazotolewa katika Kampasi ya Babati na Kampasi tarajiwa ya Songea.
Mhe. Silinde ameyasema hayo leo jijini Arusha akimwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika Mahafali ya 25 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
"Ninawapongeza kwa mpango huo, naamini utakapoanza kutekelezwa utawasaidia Watanzania; kutokana na ukweli kwamba Kilimo-biashara, Ufugaji, Ufundi na Utalii ni maeneo yanayoajiri Watanzania wengi” amesema.
Aidha, Mhe. Silinde ametoa wito kwa Taasisi za elimu ya Juu kuisaidia jamii na serikali kwa kuanzisha mitaala inayoakisi mazingira halisi ya Watanzania, itakayowawezesha kutumia elimu, ujuzi na maarifa watakayopata kutatua changamoto za Watanzania na kusaidia kukuza uchumi wao na wa nchi pia.
Pia amewaasa wahitimu wakatumie vema elimu, ujuzi na maarifa mliyoyapata kwa faida yao na ya wengine.
Naye Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema misingi ya IAA ni umahiri na weledi (excellence and professionalism), huku akiihakikishia serikali kwamba IAA itaendelea kuanzisha kozi za kimkakati zinazoendana na mahitaji ya soko na vipaumbele vya nchi.
Prof. Sedoyeka ameongeza kwamba mpaka sasa Chuo kina jumla ya kozi 71, ambapo kati ya hizo kozi 16 ni ngazi ya Astashahada, kozi 17 ni za stashahada, kozi 24 za shahada na shahada ya uzamili ni kozi 14.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, CPA. Joseph Mwigune amesema idadi ya wahitimu kwa mwaka 2023 imeongezeka kutoka wahitimu 3529 mwaka 2022 na kufikia wahitimu 5387; kati yao wahitimu wa shahada ya uzamili ni 1139, shahada 1027, stashahada 1260 na astashahada 2061.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wa shahada Bw. Shedrack Sebastian ameshukuru Uongozi wa Chuo kwa kuhakikisha wanapata elimu bora, "Tulifika IAA hatuna kitu tunaondoka tukiwa vijana mahiri wenye utayari wa kulitumikia taifa letu tunawashukuru”.
Post A Comment: