Na Okuly Julius-Dodoma
Mhandisi Ujenzi katika Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Geofrey Mwakasenga amesema uwepo wa sheria ya majengo nchini utawezesha kuwepo kwa mfumo wa pamoja wa usimamizi wa ujenzi wa majengo wenye uwezo wa kudhibiti uharibifu wa mazingira, ubora, usalama na afya.
Mhandisi Mwakasenga ameyasema hayo leo Desemba 21,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea masuala muhimu kuhusu sheria ya majengo nchini ambapo NCC inaratibu uandaaji wake.
"Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi,iliamua uandaliwe mfumo Bora wa kisheria wenye kanuni na miongozo inayojitosheleza utakaotumika katika usimamizi wa Ujenzi wa majengo nchini, kwani kwa sasa Ujenzi wa majengo unasimamiwa na sheria nyingi mbalimbali, kwa kukosekana kwa Sheria Moja Maalum,hivyo kusababisha usumbufu katika uendelezaji wa majengo na gharama zisizo za lazima kwa waendelezaji Majengo," amesema Mwakasenge
Amesema baadhi ya sheria zinazosimamia ujenzi wa majengo nchini ni pamoja na sheria za mipango miji, afya na usalama mahali pa kazi, zimamoto na uokoaji, mazingira, ukandarasi na usajili pamoja na sheria zinazosimamia taaluma na wanataaluma katika fani ya za uhandisi, ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi.
“Sheria hizi zinatoa mwongozo katika baadhi ya maeneno na kuyaacha mengine bila usimamizi, jambo linaloifanya sekta ndogo ya ujenzi wa majengo inayohusiana pia na ubomoaji wa majengo kutosimamiwa ipasavyo,”amesema.
Ameongeza kuwa mbali na jukumu ambalo baraza hilo limepewa la kuratibu uandaaji wa sheria ya majengo pia wana majukumu mengine ya kisheria inayotekeleza ikiwemo kuhamasisha na kuweka Mikakati ya kukuza,kuendeleza na kupanua sekta ya Ujenzi nchini na kushauri Serikali juu ya Maendeleo ya Sekta ya Ujenzi nchini na kuandaa mapendekezo ya utekelezaji wake.
Jukumu lingine la Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ni kutoa ushauri na msaada wa Kitaalamu kwa wadau wa Sekta ya Ujenzi kuhusu mambo yanayohusiana na sekta ya Ujenzi pamoja na kuratibu na kuwezesha utatuzi wa migogoro inayotokea katika miradi ya Ujenzi Kwa ufanisi.
Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ni Chombo kinachohusika na Uratibu wa Sekta ya Ujenzi nchini,pamoja na uchagizaji wa Maendeleo ya Sekta hiyo kwa ujumla,Baraza hili lipo kwa mujibu wa Sheria na lilianzishwa Mwaka 1979 kwa sheria ya Bunge Na 20,ambapo Baraza hilo likaanza kutekeleza majukumu yake rasmi mwaka 1981.
Post A Comment: