Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiziagiza sekta zote nchini kuhakikisha zinawatumia wataalam wa Ununuzi na Ugavi wenye sifa kwenye shughuli zao, wakati wa Kongamano la 14 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi linalofanyika katika ukumbi wa AICC, jijini Arusha.
Na. Peter Haule, WF, Arusha
Serikali imewaagiza waajiri wa Sekta zote nchini kuhakikisha wataalam wanaofanya shughuli za ununuzi na ugavi wanakuwa na sifa sitahiki kama ilivyoainishwa kwenye Sheria Na. 23 ya mwaka 2007 iliyoanzisha Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), pamoja na miongozo inayotolewa.
Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akifungua Kongamano la 14 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi linalofanyika katika ukumbi wa AICC, jijini Arusha.
Dkt. Nchemba alisema kuwa anasikitishwa na kuwepo kwa baadhi ya Wataalam wanaofanya kazi pasipo kuwa na sifa stahiki na bila kusajiliwa na Bodi kama ilivyo takwa la kifungu cha 11 cha Sheria ya PSPTB.
“Changamoto ya kuwapo kwa wataalam ambao wanafanyakazi pasipo sifa stahiki kwa sehemu kubwa inachangiwa na waajiri kuruhusu kazi za ununuzi kufanywa na waajiriwa nje ya taaluma ya ununuzi na ugavi ambayo kwa ukubwa wake inazigusa Ofisi ya Rais TAMISEMI yenye watumishi wengi zaidi wa kada hii, Ofisi ya Rais Utumishi ambao wanasimamia masuala ya ajira pamoja na Wizara Fedha kama mlezi wa kada ya ununuzi na ugavi”, alieleza Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alimwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kushirikiana na Bodi ya PSPTB, kukutana na Katibu Mkuu TAMISEMI, Katibu Mkuu Utumishi kwa utatuzi wa changamoto hiyo ili kuhakikisha kazi za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalamu wenye sifa na waliosajiliwa na Bodi kwa mujibu wa Sheria ya PSPTB.
Aidha, Dkt. Nchemba alimwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kuangalia uwezekano wa kuisaidia PSPTB kupata fedha ili iweze kufanikisha majukumu ya utekelezaji wa baadhi ya majukumu yake kisheria ikiwa pamoja na kufanya ukaguzi wa wataalam wake nchi nzima katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Vile vile Bodi hiyo iweze kuwajengea uwezo wataalam na wadau kwenye mnyororo wa ununuzi na ugavi na kufanya utafiti wa kitaaluma unawoweza kuleta ufumbuzi wa usimamizi bora wa mnyororo wa ununuzi na ugavi mambo ambayo hayafanyiki ipasavyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Pia Dkt. Nchemba ameipongeza PSPTB kwa kuendelea kusimamia maadili na mienendo ya Wataalam kwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa wataalam wanaokiuka miiko ya taaluma yao, likiwamo suala la kufanya kazi chini ya kiwango kama ilivyobainishwa kupitia taarifa ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (GAG).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PSPTB, Bw. Jacob Kibona, alisema kuwa mfumo wa usajili wa wataalam wa ununuzi na ugavi kwa njia ya mtandao unasomana na Mfumo wa Taifa wa ununuzi (NeST) ili kuhakikisha shughuli za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalam wenye sifa stahiki waliosajiliwa na PSPTB.
Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia udhibiti wa weledi wa wataalam kuhakikisha wataalam wanaotumia mfumo huo ni wenye sifa za kitaaluma na waliosajiliwa na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Bw. Godfred Mbanyi, amesema kuwa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wanawajibu mkubwa kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kufanyakazi kwa weledi na uadilifu.
Alisema kuwa mazuri ambayo Serikali imeonesha nia ya kuyatekeleza kwa wataalam hao ikiwa ni pamoja na kuongeza maslahi yao ni lazima yalipwe kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi na pia litakuwa suala la kukatisha tamaa kwa viongozi ikiwa kada hiyo inathaminiwa lakini kunabaadhi wanafanyakazi kinyume na miiko ya taaluma zao.
Kongamano la 14 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi nchini, linafanyika kuanzia Desemba 12 hadi 15 mwaka 2023 likilenga kupunguza changamoto zilizopo kwenye fani ya ununuzi na ugavi kwa kuzingatia matumizi ya kidigitali na kuhakikisha Kuna kuwa na ununuzi wenye tija.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) akiwa ameshika tuzo ya ushiriki wa Kongamano la 14 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi linalofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa - AICC, jijini Arusha, alilokabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bw. Jacob Kibona
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akimkabidhi tuzo Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Zanzibar, Bw. Arafat Haji, ambapo Shirika hilo ni mdhamini mkuu wa Kongamano la 14 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi linalofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa - AICC, jijini Arusha.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) Bw. Jacob Kibona (wa sita kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya PSPTB na viongozi wa Mkoa wa Arusha kabla ya kuanza kwa Kongamano la 14 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi linalofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa - AICC, jijini Arusha.
Post A Comment: