Na John Walter-Manyara

Wizara ya afya imetangaza kujenga Kituo kipya cha afya katika eneo la Warreta lililotengwa na Serikali kwa ajili ya Ujenzi wa makazi mapya kwa watu walioathiriwa na maporomoko ya udongo, matope, mawe na magogo kutoka Mlima Hanang' mkoani Manyara.

Uamuzi huo umetangazwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akiwa Wilayani humo kutoa pole kwa Waathirika wa janga hilo lilisababisha vifo vya watu 89 . 

Akiwa katika kitongoji  cha Gendabi  kilichoharibiwa na janga hilo, Waziri Ummy amesema wizara yake itatoa shilingi milioni mia tano (500)  kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Kituo hicho.

Ili kuongeza nguvu ya utoaji huduma kwa mkoa wa Manyara ulioathiriwa na janga hilo, Ummy amesema wizara yake itapeleka magari Matatu ya kubebea wagonjwa kama sehemu ya mchango wa wizara yake kwa Wananchi wa Hanang'. 

Kwa upande wake Mkuu wa wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameshukuru wizara ya afya Kwa namna walivyojitoa kudhibiti magonjwa ya mlipuko wakati wa janga hilo ambalo lilisababisha maji taka kusambaa maeneo mbalimbali. 

Kuhusu eneo la makazi mapya, Mkuu wa mkoa amesema kazi ya kupima viwanja katika eneo hilo lenye ekari 100 tayari limekamilika ambapo viwanja 259 vya makazi na Biashara vimeshatengwa na kinachosubiriwa Sasa ni maelekezo ya ofisi ya  Waziri Mkuu kitengo cha maafa ili kuanza Ujenzi. 

Wizara ya afya pia imeuhakikishia umma kuwa itaendelea kugharamia matibabu ya Majeruhi watano wanaoendelea kupatiwa matibabu. 


Share To:

Post A Comment: