WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali iko kwenye maandalizi ya awali ya ujenzi wa kampasi 14 mpya za vyuo vikuu kwenye mikoa ya pembezoni isiyokuwa na vyuo vikuu.
Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Kigoma, Ruvuma, Singida, Mwanza, Kagera, Tanga, Njombe, Tabora, Manyara, Simiyu, Shinyanga, Lindi, Rukwa, na Katavi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 30, 2023) wakati akizungumza na wahadhiri na wahitimu kwenye mahafali ya 26 ya Chuo Kikuu cha Iringa yaliyofanyika chuoni hapo amako pia alimwakilisha Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan.
“Hatua hiyo ni moja ya jitihada za makusudi za Serikali za kuharakisha ukuaji wa uchumi kwenye maeneo ya pembezoni, kuongeza nafasi za elimu ya ufundi, ujuzi na stadi za maisha katika maeneo hayo ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fursa za elimu na ajira.”
Akielezea uboreshaji wa miundombinu ya vyuo vikuu, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inaendelea na ujenzi wa miundombinu muhimu ambayo ni vyumba vya mihadhara, maabara, nyumba za walimu na maktaba.
“Kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Serikali inaendelea na ujenzi wa mabweni 34; vyumba vya mihadhara na madarasa 130; kumbi za mikutano ya kisayansi 23; maabara/karakana za kufundishia 108; miundombinu ya shambani na vituo atamizi 10.
Amesema kukamilika kwa ujenzi huo kunatarajiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma programu za kipaumbele (STEM) kutoka wanafunzi 40,000 kwa mwaka 2020 hadi kufikia 106,000 mwaka 2026.
Kuhusu ombi la kujengewa bweni la wasichana litakaloitwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema amelichukua na ltaenda kufanyiwa kazi Serikalini.
Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo aliwatunuku wahitimu 1,994 wakiwemo 108 wa shahada za uzamili wa elimu (Ualimu), Utawala na Usimamizi wa Biashara, Sanaa ya Maendeleo ya Jami na Usimamizi wa Miradi, Sayansi katika Saikolojia Nasihi, Misheni na Maendeleo ya Jamii, Sheria za Habari na Mawasiliano ya TEHAMA, na mfumo wa sheria za Jinai za Kimataifa na Haki za Binadamu.
Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, CPA. Lilian Badi Manara alisema wanamuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan awasaidie kujenga bweni la wanachuo wa kike kwani wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa kifedha.
“Kutokana na changamoto ya upungufu wa kifedha, tuna upungufu wa mabeni na hasa wa kike. Na matokeo yake baadhi wanalazimika kuishi mitaani ambako wanakutana na ukatili wa kijinsia na baadhi wanalazimika kuingia kwenye ndoa za muda mfupi,” alisema.
Post A Comment: