Na John Walter-Babati
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema zoezi la kuhakiki waathiriwa wa maafa ya maporomoko ya udongo,mawe na magogo Hanang' linaendelea ili kuwathibiti wasiokuwa waaminifu wanaotaka kujinufaisha kupitia misaada inayotolewa na serikali kupitia wadau mbalimbali.
Mkuu huyo wa mkoa ameelekeza zoezi hilo lifanyike kwa uwazi kuwatambua walioathiriwa na maafa hayo yaliyotokea Desemba 3 mwaka huu.
Sendiga amesema kuwa ofisi za kata zitakuwa vituo vya kutolea misaada na kuwaelekeza waathiriwa wa maafa ambao hawajaorodheshwa kama waathirika wanaohitaji kuendelea kupatiwa misaada, kufika katika ofisi hizo kujiandikisha.
Katika hatua nyingine matumaini ya maisha ya awali kwa wananchi wa wilaya ya Hanang' yamerejea huduma mbalimbali kama maji zimerejea ambapo mkuu wa mkoa anasema serikali inaendelea kurejesha huduma katika maeneo ambayo bado huduma hizi hazipo.
Kwa upande wa miundombinu, Sendega amethibitisha ujenzi wa soko jipya kwani eneo la mwanzo katika soko la zamani limebainika kuwa katika mkondo wa maji.
"Tunajenga soko lingine kwa sababu lile soko lililopo pale pameonekana ndio mkondo mkubwa wa maji unapita, maji yameshatengeneza njia pale yawezekana yakarudi tena kesho au keshokutwa, kwa hiyo tumeanza sasa hivi miundombinu ya utengenezaji wa soko lingine ambalo tuna imani ndani ya muda mfupi litakuwa tayari na wananchi watarudi kuendelea kufanya shughuli zao" amema mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga.
Post A Comment: