Wananchi wa Mitaa ya Mapinduzi A na B kata ya Ngh’ongh’ona,Jijini Dodoma wameishukuru serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia S. Hassan na Mbunge Mh. Anthony Mavunde kwa kutimiza ahadi ya ujenzi wa shule ya Sekondari katika eneo hilo la Mapinduzi ikiwa ni namna ya kuboresha sekta ya Elimu Jijini Dodoma.
Shukrani hizo zimetolewa wakati wa ziara ya Mbunge Anthony Mavunde kukagua shughuli za maendeleo katika kata ya Ngh’ongh’ona.
Akitoa maelezo ya awali Diwani wa Kata ya Ngh’ongh’ona Mh. Loth H. Loth amesema watoto wa eneo hilo hutembea kwa zaidi ya kilomita 15 kwenda shule ya Sekondari ya Ngh’ongh’ona na hivyo kusababisha watoto wengi wa kike kukatisha masomo yao kwa kupata ujauzito,hivyo ujenzi wa shule hiyo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Mapinduzi.
Akizungumza na Wananchi hao Mbunge Anthony Mavunde amesema ni dhamira ya serikali kuhakikisha kwamba inaboresha na kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi hivyo ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Mapinduzi ni ishara tosha juu ya dhamira ya dhati ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan ya kukuza sekta ya Elimu Jijini Dodoma.
Katika kuhakikisha Shule hiyo inaanza kutoa huduma mapema mwezi Januari 2024,Mbunge Mavunde pia amechangia Tsh 10,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo na kuahidi kujenga darasa 1 kuunga mkono juhudi za serikali.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Dodoma Cde. Charles Mamba amewahakikishia wananchi kwamba CCM itaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani kwa ukamilifu ili serikali na viongozi wa kuchaguliwa wawajibike ipasavyo katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika ziara hiyo pia Mbunge Mavunde alipata nafasi ya kukagua kivuko kinachounganisha eneo la Ngh’ongh’ona na Chuo kikuu cha Dodoma na kuwataka TARURA kukamilisha kazi kwa uharaka katika eneo hilo.
Post A Comment: