Serikali chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi cha shilingi trilioni 6.7 kwaajili ya kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu ndani na nje ya nchi ili wananchi wengi waweze kupata matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akiongea na wananchi waliofika katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kwaajili ya kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo.

Dkt. Mollel ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Siha alisema katika kambi hiyo kwa muda wa siku tatu wataalamu wameona watu 307 kati yao 37 wamekutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

“Kama hawa watu waliogundulika kuwa na matatizo wasingeonwa katika kambi hii si ajabu wasingeweza kuishi muda mrefu lakini uwepo wa matibabu haya umewasaidia kugundulika kuwa na mamtatizo ambayo yanahitaji matibabu ya kibingwa na watapata matibabu mapema”, alisema Dkt. Mollel.

“Huduma za matibabu zinazopatikana katika upimaji huu zinatolewa bila malipo yoyote yale kwani Serikali imegharamia kila kitu na kutokana na uhitaji kuwa mkubwa JKCI wameongeza siku mbili hivyo basi kambi hii itamalizika siku ya Jumapili, ninawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kuja kupima afya zenu”, alisisistiza Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya na hivyo kuwafanya watanzania na ambao siyo watanzania kuwa na uhakika wa kupata matibabu ya kibingwa na ndiyo maana Tanzania inapokea wagonjwa kutoka nchi za jirani ambao wanakuja kutibiwa hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa JKCI Dkt. Delilah Kimambo alisema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ya kuwafuata wananchi mahali walipo na kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Pia katika tiba mkoba wanatoa nafasi kwa wale wanaokutwa na matatizo ya moyo kupata nafasi ya kutibiwa mapema kwa kupewa rufaa na kuwajengea uwezo wataalamu wa hospitali husika ili baada ya kumalizika kwa kambi ya matibabu nao waweze kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo.

 

Share To:

Post A Comment: