Na Joel Maduka,Geita

Nyumba 556 za makazi ya watu katika tarafa ya Kasamwa  kata za  Kasamwa,Shiloleli Bulela na Kanyara  Wilayani  Geita zimepata madhara kufuatia mvua zilizonyesha  zikiambatana na upepo na kusababisha baadhi ya nyumba kuanguka na zingine kubomoka kutokana na kushindwa kuimili maji.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa maafa  wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Valeria Makonda  wakati wa  hafla ya ugawaji wa msaada kwa waathirika wa mafuriko ndani ya halmashauri hiyo.

Amesema Mkoa wa Geita tayari umepokea tani 22.1 za mahindi pamoja na vifaa vya msaada wa kibinadamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kaya ambazo makazi yao yaliharibiwa na mvua ikiwemo za halmashauri ya Mji wa Geita.

Valeria amebainisha miongoni mwa wanufaika wa msaada wa mahindi hayo ni waathirika wa nyumba hizo za makazi zilizoharibiwa na mvua, ambapo waathirika wamepatiwa msaada wa vyakula na malazi vilivyotolewa na serikali.

Katika taarifa yake kwa Mkuu wa wilaya Mratibu huyo wa Maafa ameeleza kuwa mpaka sasa kiasi cha Sh milioni 225.46 kinahitajika ili kukarabati miundombinu ya taasisi za umma zilizoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe akizungumza baada ya kugawa vifaa vya kibinadamu, amewataka wananchi kuzingatia suala la usalama kwa kujenga maeneo ambayo yapo salama.

“Niwaombe ndugu zangu tuzingatie suala la kujenga makazi sehemu ambazo ni salama kuna watu wamekuwa wakijenga majarubani pindi mvua zikiwa hazinyeshi suala ambalo ni hatari kwa miasha yenu ninawaomba tuchukue taadhari ndugu zangu”Cornel Magembe Mkuu wa WIlaya ya Geita..


Share To:

Post A Comment: