Katibu Mtendaji wa NACTVE, Dkt. Adolf Rutayuga akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa NACTVET katika Maonesho na Maadhimisho ya Miaka 50 ya NECTA yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), linashiriki Maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani Tanzania ( NECTA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja, Dar es Salaam.
Akizungumza katika maonesho hayo,leo tarehe 30 Novemba 2023, Katibu Mtendaji wa NACTVE, Dkt. Adolf Rutayuga amesema, NECTA ni wadau wakubwa sana wa NACTVET kwani wanafunzi wengi wanaojiunga na vyuo vya kati ni wale waliomaliza masomo ya kidato cha nne yanayoratibiwa na NECTA.
Amebainisha kwamba kwa kutumia kanzidata ya NECTA inayosomana na ile ya NACTVET, inawezesha utambuzi wa wanafunzi wenye sifa stahiki kuwawezesha kujiunga na vyuo vya kati na hivyo ushiriki wa NACTVET umelenga kuunga mkono na kupongeza mafanikio makubwa ya NECTA katika utoaji wa huduma kwa jamii.
Aidha, Dkt Rutayuga amesema, NACTVET imeshiriki maonesho hayo ili kukutana na wadau mbalimbali ili kutoa elimu juu ya majukumu yake na kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yanayosimamiwa na kutekelezwa na Baraza.
Ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wadau na wananchi wote kwa ujumla kutembelea banda la NACTVET wakati huu wa Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya NECTA , yaliyofunguliwa rasmi leo tarehe 30 Novemba, 2023 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ambapo yatadumu kwa siku nne hadi tarehe 3 Desemba 2023.
Baadhi ya Matukio ya katika Banda la NACTVET kwenye Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya NECTA yanayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Post A Comment: