KAIMU Mkuu wa Idara ya Ardhi, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Bw.Deo Damian Msilu,akizungumza na waandishi wa habari mara baada kukagua maeno yaliyopitiwa na Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) Katika kata mbili za Pera na Bwilingu.
MENEJA wa Mradi kwa Chalinze Bi.Rogathe Jonson Kaale,akizungumza na waandishi wa habari mara baada kukagua maeno yaliyopitiwa na Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) Katika kata mbili za Pera na Bwilingu katika Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani.
Na Alex Sonna-CHALINZE
IMEELEZWA kuwa utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) kwa Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani umekuwa mwarobani wa changamoto zilizokuwa zikiwasumbua wananchi kutokana na kutopimiwa maeneo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Deo Msilu, amesema mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi ambao walikuwa wakililia kupimiwa maeneo yao lakini walikuwa hawapimiwi.
“Mradi huu umekuja kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha hivyo tumeweza kufanikiwa kupanga hasa eneo la katikati ya Mji, mradi huu unalenga kupima viwanja 10,000 lakini malengo yetu ni viwanja 50,000, kupitia mradi huu tumetatua migogoro mingi ya ardhi ”amesema.
Naye,Meneja wa Mradi kwa Chalinze Bi.Rogathe Kaale,amesema mradi huo walianza rasmi Juni 27, 2023 ulianza kwa kutambulishwa ngazi ya mkoa, wilaya na viongozi wa halmashauri na kata mbili za Pera na Bwilingu vinakadiriwa kupimwa viwanja 10,000.
“Tulianza kwa mikutano ya hadhara ambapo wananchi walielimishwa umuhimu wa mradi huu baada ya hapo tuliteua kamati za urasimishaji kwa mujibu wa mwongozo wa urasilimishaji wa wizara ya ardhi na baada ya kamati tukaanza kukusanya taarifa, tulikuwa na timu ya Wapima na Surveyor tufanya zoezi kwa miezi mitatu kwenye kata hizi tulipata vipande 11,000 kwasababu lengo letu lilikuwa viwanja 10,000 tukaanza zoezi la upimaji linalofanywa kwa njia shirikishi kwa kuwashirikisha wananchi kuanzia ngazi ya chini,”amesema.
Amesema ramani za mipango miji zilizoandaliwa zimeunganishwa na ramani za anga ili wananchi waone nyumba zao, barabara na maeneo yaliyopendekezwa.
“Katika zoezi hili mwananchi akichangia barabara lazima asaini fomu kuonesha ameridhia eneo lake limetolewa kwa matumizi ya barabara ili kwa hapo baadae lisijetumika kwa matumizi mengine tofauti na tuliitisha mikutano na kubandika ramani wananchi walihakiki taarifa zao na hadi sasa 5000 wamehakiki taarifa zao kuwa wameridhia mpango ulioandaliwa kuwa ni sahihi hatua za upimaji ziendelee,”amesema.
Amesema viwanja 7500 zimepimwa na vipo katika hatua za mwisho kuidhinishwa na michoro ya mipango miji iliyoandaliwa ipo 50 ya viwanja vya matumizi mbalimbali kulingana na wananchi walivyoshauriwa.
“Tumejipanga hadi mwisho wa mwezi huu tuwe tumepima na kuidhinisha ramani viwanja 10,000 ili mwakani Januari tuhamie hatua ya umilikishaji ambapo kila mwananchi atakuja kuhakiki kiwanja chake kama alivyoridhia mwanzo, uzuri kwasasa gharama za umilikishwaji zimepungua zipo nusu ya zile za awali tunaamini wananchi wana uwezo wa kulipia,”amesema.
Kadhalika, amesema Mwezi Februari 2024 wataendelea na awamu ya pili ya kupima na kumilikisha viwanja 20,000 na ndo malengo ya halmashauri waliyopewa.
“Changamoto hazikosekani kuna changamoto za migogoro imekuwa ikiibuka tumekuwa tukiitatua kwa kushirikisha wataalaamu wa ardhi, wananchi na madiwani na tunaingiza kwenye kanzidata ili kusitokee usumbufu kwenye umilikishaji,”amesema.
Post A Comment: