Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amewatembelea na kuwapa pole wananchi wa Kata ya Mbabala ambao walipata athari ya mvua kubwa iliombatana na upepo mkali iliyoleta athari kwa nyumba 259 ambazo baadhi zimebomoka na nyingine kuezuliwa paa hivyo kupelekea idadi kubwa ya watu kukosa makazi na mwananchi mmoja kupoteza maisha.
Akitoa taarifa ya athari hizo Mtendaji wa Mtaa wa Nguji-Mbabala Ndg. Jumanne Misanga Njiku alieleza kuwa mnano mwezi Novemba mwishoni na Tarehe 5 Desemba 2023 mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilileta athari kubwa kwa wakazi wa mitaa mitatu ya Kata ya Mbabala na kuwasabishia hasara kubwa ya mali ikiwemo upotevu wa mifugo na kupelekea kifo cha mama aliyekuwa amelala pamoja na watoto wawili ambao walidondokewa na nyumba na hivyo Bi. Rahel Nguselo kupoteza maisha na kuwaacha watoto wawili wadogo.
Akiwa hapo Mbunge Mavunde ametoa pole kwa wananchi wote waathirika kwa kadhia hii kubwa na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa kwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hivi sasa kama ambavyo imetabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Aidha,Mbunge Mavunde amejitolea kujenga nyumba akishirikiana na ofisi ya CCM Mkoa Dodoma kwa ajili ya watoto wawili wa darasa la kwanza ambao mama yao alifariki kwa kudondokewa na nyumba hivyo kuwafanya kukosa makazi,na pia kutoa msaada kwa waathirika wa tani 2 za mahindi,magodoro 50,sukari,maharage kilo 200 na Maji katoni 100.
Aidha,Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Dodoma Cde. Charles Mamba ametoa pole kwa waathirika wa majanga haya ya mvua na kuendelea kusisitiza juu ya kuchukua tahadhari kwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya Nchi.
Akishukuru kwa niaba ya waathirika Bi. Hawa Hassan Myika amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kuwakimbilia na kuwajali katika kipindi hiki kigumu na kuiomba serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa kuwasaidia ili warudi katika hali yao ya kawaida ya maisha ya kila siku.
Post A Comment: