KATIKA kuadhimisha Miaka 75 ya Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania na Jaji mstaafu Bw. Mathew Mwalimu amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotoa haki za binadamu kwa kuridhia mikataba ya kimataifa na kikanda pamoja na kutunga sera mbalimbali na Sheria ili kusaidia jamii.
Ameyasema hayo leo Desemba 14,2023 Jijini Dar es Salaam, walipokutana na wadau mbalimbali na kufanya tathimini ya kutambua mafanikio waliyo yafikia na kubainisha changamoto ambazo zimejitokeza katika vipindi mbalimbali kwa lengo la kuzitatua ili kulinda haki za Binadamu.
Aidha ametoa wito kwa wabunge wanapotunga Sheria kufuata misingi ya haki za binadamu ambazo zitasaidia katika utoaji wa haki kwa watu wote ili kulinda utu wa mtu anayedai haki bila kuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.
"Lazima watanzania tubadilike mitazamo, haki za binadamu ni kitu ambacho hauwezi kukishika ukasema hii ni haki za binadamu, haki za binadamu tunaishi nazo kwa kuheshimiana kwa kuangalia utu wetu, mtu asipoheshimiwa inamaana unavunja utu wake". Amesema Bw. Mathew
Amesema Sheria zinazotungwa zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi wakidai, wabunge wanazilalamikia pia na ameeleza kuwa wabunge ndio wanaotunga sheria wanategemea wabunge wawe makini wanapotunga sheria ili kuhakikisha Sheria haziwezi kukiuka misingi ya haki za binadamu.
Pamoja na hayo amewaasa wadau wa haki za Binadamu kuungana ili kuzungumza lugha moja katika utetezi wa haki za watu,na kushiriki katika kutoa elimu kwa jamii ya watanzania katika mikoa yote ili kkushiriki katika masuala ya kulinda utu na haki za Binadamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga ametoa wito kwa vijana kushiriki kikamilifu katika michakato ya kitaifa hasa katika kupambania haki za binadamu ili kuweka uwiano sawa kwani vijana ni kundi lenye nguvu.
"Ninatamani kuwe na sera bora kwa ajili ya vijana, najua kuna sera mbalimbali kwa ajili ya vijana ila kuwepo na sera za mafunzo kwa ajili ya kutetea haki zao na haki za binadamu". Wakili,Anna Amesema
Aidha Wakili Anna ameeleza kuwa kunatakiwa kuwa na mapitio ya sheria zile zilizotungwa zamani ili ziundwe upya kwani sheria hubadirika kulingana wakati ili kusaidia haki itendeke.
"Sheria zinabadirika badirika, kuna sheria ilikuwepo mwaka 1971 mtoto wa kike wa miaka 13 alikua anaweza kuolewa ila leo haiwezekani, maana bado yuko shuleni, Sheria nyingi zimepitwa na wakati kwakweli hivyo tunapaswa kuzifanyia marejeo". Wakili Anna Amesema.
Naye Msaidizi wa Mkuu Kitengo cha Idara ya Habari Kituo Cha Runinga Cha ITV Bw. Isack Mpayo amesema kuwa vyombo vya habari ni wadau wakubwa wa utetezi wa haki za binadamu ambapo wamekutana na watu ambao wanajua haki zao lakini kuna wakati zinacheleweshwa vyombo vya habari vimetumika kupaza sauti ili haki iweze kupatikana.
Aidha Bw.Mpayo amebainisha kuwa bado kunachangamoto ambayo inahafifisha uwasilishaji wa habari zinazohusu haki za binadamu kutokana na sera na sheria ambazo zikifanyiwa marekebisho zitaondoa kuminywa kwa haki.
"Bado vyombo vya habari vinatumia nguvu kuwasilisha, bado kunasheria ambazo hazijarekebishwa ambazo zinaminya haki za watu na kwa uhuru wa vyombo vya habari ambazo zikirekebishwa zitatoa nafasi ujumbe uwzee kufika vile ipasavyo". Amesema Bw. Mpayo
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania na Jaji mstaafu Bw. Mathew Mwaimu akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Haki za Binadamu katika Kuadhimisha Miaka 75 ya Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu lililofanyika leo Desemba 14,2023 Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya wadau wa Haki za Binadamu wakiwa katika Ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Haki za Binadamu katika Kuadhimisha Miaka 75 ya Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu lililofanyika leo Desemba 14,2023 Jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania na Jaji mstaafu Bw. Mathew Mwaimu akipata picha ya pamoja na wadau mbalimbali wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Haki za Binadamu katika Kuadhimisha Miaka 75 ya Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu lililofanyika leo Desemba 14,2023 Jijini Dar es Salaam
Post A Comment: