Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Rashid Nchimbi ametoa wito kwa wanachuo wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) wilayani Monduli kutosita kutoa taarifa pindi mmojawao atafanyiwa vitendo vya Ukatili wa Kijinsia.

Hayo aliyasema mchana wa leo katika ukumbi wa chuo hicho, ambapo zaidi ya wanachuo 350 walihudhuria.

ASP. Nchimbi alisema kwamba, baadhi ya watu bado hawajafahamu mgawanyo wa majukumu kati ya huduma za kawaida na zile zitolewazo na Dawati la Jinsia na Watoto.

 "Baadhi ya watu wamekuwa na shaka kuhusiana na mazingira ya utoaji wa taarifa zao pale kituoni, hali inayopelekea pengine kusita kabisa kutoa taarifa.

"Napenda kuwahakikishia kwamba, Jeshi la Polisi wilaya ya Monduli tuna ofisi ambayo ina askari wenye mafunzo maalum ambao huwa  wanampokea mhusika na kuongea naye kwa unyeti wa hali ya juu; hivyo msisite kuja kuripoti". Alifafanua ASP Nchimbi.

ASP. Nchimbi alisema, maofisa na askari wa Dawati la Jinsia na watoto wana mafunzo maalum lakini pia huwa wanapatiwa semina za mara kwa mara ili waendelee kuwa wajuzi katika  kumhudumia mtu aliyepatwa na matatizo hayo ikiwa ni pamoja na kumhoji kwa usiri.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto wilayani Monduli Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Jacqueline Uhwelo, aliwakumbusha wanafunzi hao kuzingatia kilichowapeleka chuoni hapo ili waweze kutimiza malengo yao.

Aliwaasa hasa wasichana kujitambua na kutojiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi hali ambayo inaweza kuwasababishia mifarakano na mimba zisizotarajia.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Utawala, Fedha na Mipango Bw. Elidaima Kanda, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu hiyo na kuahidi kutoa nafasi za mara kwa mara kwa Jeshi hilo ili waweze kuwaelimisha na kuwapa mwanga wanachuo hao ambao wengi wao wanaishi uraiani.

Alisema Dunia hivi sasa imezidi kubadilika ambapo zamani Ukatili ulikuwa unafanywa na watu wa nje ya familia lakini hivi sasa hadi mzazi anaweza akamfanyia mtoto wake vitendo vya Ukatili.




Share To:

Post A Comment: