Na Issa Sabuni na Beatrice Lyimo
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali ipo kazini kuhakikisha suala la kukatika kwa umeme linashughulikiwa kikamilifu na hakuna hujuma yeyote kama ambavyo inasemekana.
Naibu Waziri Kapinga ameyasema hayo tarehe 08 Desemba, 2023 wakati akijibu swali ya mwananchi wa Kijiji cha Masimba, Kata ya Tongwe wilayani Muheza kuhusu kukatika kwa umeme huo kijijini hapo.
“Ninakubaliana na yeye kuwa umeme unakatika kwa kuwa tunapitia kipindi cha mgao wa umeme, lakini niwahakikishie ndugu zangu, Mheshimiwa Rais alitupa miezi sita kuhakikisha tunaondoa mgao wa umeme, tupo kazini na kwa mipango ambayo tunayo tunategemea ndani ya miezi sita hiyo tutakuwa tumeshaondoa mgao wa umeme, miezi sita inaisha mwezi wa tatu 2024, mpaka kufikia hapo na kwa mipango iliyopo miradi ambayo Mheshimiwa Rais ametupatia fedha tunatekeleza tunategemea tutaondoka kabisa kwenye mgao wa umeme”
“Kwa kipindi hiki mvua zinanyesha, maeneo kwa maeneo, maeneo ambayo tunafanya uzalishaji wa umeme kule kwenye mabwawa yetu ya umeme Kidatu, Kihansu na Mtera ndio mvua zimeanza kwa hiyo tunategemea kadiri mvua zinavyoendelea kunyesha, maji yanavyoendelea kujaa tutakuwa tumepunguza tatizo kwa kiasi kikubwa hivyo niwaondoe shaka, hakuna hujuma inayofanyika kama ambavyo inasemwa Watu wanauza majenereta, sola hapana, Serikali ipo kazini na tunaangaliza jicho kwelikweli”. Alisema Naibu Waziri Kapinga.
Aidha amebainisha kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha inatoa huduma bora na stahiki ya upatikanaji wa umeme ambao ni wa kudumu na utawasaidia Wananchi kwenye shughuli za maendeleo.
Mbali na hayo, Mhe. Kapinga amewasihi Wananchi kuendelea kuunganisha umeme kwenye majumba yao (wiring) ili miradi hiyo ikifika, waweze kuunganishwa, hii itasaidia kuona thamani ya Miradi ambayo inapelekwa kwenye vitongoji na vijiji hivyo.
Hata hivyo, Mhe. Kapinga amewaahidi Wakazi wa Kijiji cha Masimba kumaliza suala la usambazaji wa umeme katika vitongoji viwili vilivyobaki katika Kijiji hicho.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kutekeleza Miradi mbalimbali katika Jimbo la Muheza ili kuboresha huduma za jamii ambapo Jimbo hilo, lina Jumla ya Kata 37, Vijiji 135 na Vitongoji 522, hata hivyo vijiji vyote 135 vimepatiwa huduma ya umeme kupitia mradi wa awali wa REA III (Mzunguko wa Kwanza na wa Pili) na PERI Urbani III.
Post A Comment: