Na John Walter-Hanang'

Idadi ya Miili iliyopatikana Kufuatia Maafa ya Maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang'  wilaya ya Hanang' mkoani Manyara imefika 87.

Miili yote hiyo imeshatambuliwa na ndugu zao na kuchukuliwa kwa ajili ya mazishi.

Serikali inagharamia mazishi na kutoa mkono wa pole shilingi milioni moja kwa kila marehemu ikiwa ni  maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Taarifa ya msemaji ya mkurugenzi wa idara ya habari maelezo na msemaji mkuu wa serikali Mobhare Matinyi, jumapili desemba 9,2023  imeeleza kuwa hadi  sasa jumla ya majeruhi na wagonjwa waliopokelewa tangu maafa yalipotokea jumapili Desemba 3,2023 ni 139 na waliopo hospitalini ni 30 huku wengine isipokuwa wawili waliofariki wamesharuhusiwa na kurejea nyumbani.

Aidha wagonjwa hao 30 waliopo hospitalini wapo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara 19, Hospitali ya wilaya ya Hanang'  Tumaini 8 na kituo cha afya Gendabi wapo wagonjwa 3.

Hadi sasa waathirika 517 wamepokelewa kwenye kambi tatu zinazotoa huduma, ambapo kwa juhudi za serikali waathirika 215 wameshaunganishwa na familia zao na waliobakia kambini ni 302 na kaya 212 zipo tayari kuunganishwa na familia zao baada ya kupatiwa mahitaji muhimu ya kibinadamu.

Kila kaya inayoondoka kambini  inapatiwa chakula cha kutumia kwa muda wa siku 30 na mahitaji mengine yakiwemo mavazi.

Tayari waathirika 517 wameshapatiwa huduma za kisaikolojia kutokea kambini na wengine 721 walioko nje ya kambi. Serikali ina jumla ya maafisa ustawi wa jamii 43 wanaotoa ushauri nasaha kwa wananchi walioathirika na maafa haya.

Kila kaya inayoondoka kambini inapewa chakula cha siku 30 kwa kufuata  mwongozo wa lishe ambacho ni: unga, mchele, maharage, mafuta ya kula, sukari, chumvi, maji ya kunywa, jiko la kupikia na watoto wanapewa unga wa lishe. Vile vile, kila kaya inapewa godoro, blanketi, duveti, shuka, sufuria, nguo za ndani, taulo za kile, pampasi za watoto, dawa za meno, miswaki, sabuni za miche na unga, sahani, vikombe, beseni na ndoo. 


Share To:

Post A Comment: