Na John Walter-Manyara
Taarifa ya Jeshi la Polisi nchini iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya jeshi hilo, imeeleza kuwa wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa mauaji ya Beatrice James Minja yaliyotokea Tarekea Wilaya ya Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.
Mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina la Lukas Paul Tarimo anadaiwa kufanya mauaji hayo Novemba 12, 2023 na kukimbia kusikojulikana.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,SACP David Misime amesema kuwa baada ya taarifa hizo kufika Jeshi la Polisi lilianza mara moja uchunguzi kumtafuta aliyefanya tukio hilo ambapo mapema leo Desemba 31,2023 jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata.
SACP Misime amesema kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa mafichoni huko Kijiji cha Jema kilichopo Kata ya Olondonyosambu Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha.
Amebainisha kuwa, baada ya mtuhumiwa kuhisi atafikiwa na mkono wa sheria alijaribu kunywa sumu ya kuuwa wadudu, lakini jeshi hilo lilifanikiwa kuwahi sehemu alipo mtuhumiwa huyo na jitihada za kumkimbiza katika kituo cha afya zilifanyika ambapo alipata matibabu na anaendelea vizuri huku akisubiri taratibu za kisheria.
Msemaji wa Jeshi hilo amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na Jeshi la Polisi kitendo kilichopelekea mtuhumiwa wa mauaji kukamatwa huku akiwaomba wananchi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.
Post A Comment: