NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Festo Dugange amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mji Nanyamba kuhakikisha kuwa ifikapo  Desemba mosi, mwaka huu Zahanati ya Mkomo inaanze kuwahudumia wananchi.

 Dkt. Dugange ametoa agizo hilo kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mtwara iliyofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

" Mhe Mwenyekiti sisi tunashukuru kwa kuwa Kamati imeridhika na ujenzi wa mradi huu wa Zahanati hivyo pia tungependa kuihakikishia kamati hii kama alivyosema Mkurugenzi wa Mji kuanzia Desemba mosi wananchi wataanza kupata huduma za afya kwenye Zahanati hii."

"Na katika hilo nimuagize Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pia kuhakikisha inapofika Desemba 5, mwaka huu anafika katika Zahanati hii ya Mkomo kuangalia kama ahadi aliyotoa Mkurugenzi ya kuanza kutoa huduma imetekelezwa kwa kuwa lengo la Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za afya bila changamoto yoyote," amesema Dkt. Dugange.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Denis Londo ameipongeza TAMISEMI kwa namna inavyotekeleza kwa weledi miradi ya afya katika Mkoa wa Mtwara na kuwataka kufanyia kazi ushauri wote uliotolewa na kamati hiyo kwenye miradi iliyotembelewa.

"Kamati tunaipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia kwa namna inavyotekeleza miradi hii ya afya kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI, rai yetu kwenu ni kufanyia kazi kila ushauri ambao umetolewa ili kuhakikisha wananchi wetu wananufaika na Zahanati hizi, Vituo vya Afya na Hospitali ambazo zimejengwa kwenye maeneo yao," amesema Mhe. Londo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imehitimisha ziara yake katika Mkoa wa Mtwara ambapo ilikagua na kutembelea mradi wa Kituo cha Afya Mtandi kilichopo Halmashauri ya Mji Masasi, Hospitali ya Wilaya Newala, Zahanati ya Mkomo na Kituo cha Afya Kitaya.



Share To:

Post A Comment: