Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezindua rasmi Mwongozo wa Taifa wa Chakula na Ulaji, uliandaliwa ili kuhamasisha matumizi sahihi ya Chakula mchanganyiko katika kutokomeza changamoto zote za Utapiamlo hapa nchini.
Akizundua Mwongozo huo Leo Novemba 16, 2023 katika Soko la Kisutu Jijjni Dar Es Salaam, Mhe. Ummy Mwalimu amesema Mwongozo huo unaweza kutumiwa na kila Mtanzania na umehakisi mazingira yaliyopo nchini, na unaenda kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 12 Barani Afrika kuwa na Mwongozo wake wa Chakula na Ulaji.
“Nimeupitia Mwongozo huu nataka niwahakikishie Watanzania Mwongozo huu unaweza kutumiwa na kila Mtanzania, awe mjini, awe kijijini, awe tajiri, awe maskini, ni mwongozo ambao unahakisi Mazingira ya Kitanzania”amesema Ummy.
Waziri Ummy amesema Watanzania wanahitaji sana Mwongozo huu kwa sababu bado kuna tatizo la lishe duni nchini na tatizo hilo limekuwa kisababishi kikubwa cha utapiamlo wa aina zote katika jamii na kuchangia kushindwa kufikia kwa malengo ya kiafya na kimaendeleo kwa mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla.
Aidha katika Hatua nyingine Mhe. Ummy Mwalimu amewataka maafisa lishe na wataalamu wa afya, Watafiti, wataalamu wanaotoa elimu ya lishe katika jamii, kuhakikisha wanatumia Mwongozo huo vizuri katika utoaji wa elimu ya masuala ya lishe, ikiwemo elimu sahihi kulingana na mwongozo unavyowataka.
Akizungumzia Matumizi ya Mwongozo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, amesema, kiu kubwa ya Watanzania ilikuwa ni kufahamu ale chakula gani na chenye mchanganyiko upi na kwa kiasi gani, hivyo ujio wa Mwongozo wa Chakula na Ulaji unaenda kukidhi mahitaji hayo.
“Matumizi sahihi ya Mwongozo huu yanaenda kuleta tumaini la kuondokana na matatizo ya udumavu na kwenda kupunguza changamoto zinazoleta matatizo ya upungufu wa Madini na Vitamini kwa Watanzania” alisema Dkt. Germana.
Post A Comment: