Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, (kulia) akiongoza upimaji wa kiwanja kilichopo eneo la Manga Manispaa ya Singida kinachomilikiwa na Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA) ambacho mfanyabiashara Philipo Masawe maarufu Medikenya aliuziwa kwa Sh.milioni 50 bila kufuata utaratibu. Kushoto ni Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro akiwa na baadhi ya viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWA)_ Mkoa wa Singida wakati wa upimaji wa eneo hilo.
......................................................................................
Dotto Mwaibale na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
WAUMINI wa dini ya kiislamu Kijiji cha Manga Kata
ya Mtipa Manispaa ya Singida wametoa onyo kwa baadhi ya watu wakiwamo waumini
wa dini hiyo wanaendeleza malumbano na upotoshaji kuhusu mgogoro wa kiwanja
kilichopo eneo la Manga Manispaa ya Singida kinachomilikiwa na Jumuiya ya
Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA) ambacho mfanyabiashara Philipo Masawe maarufu
Medikenya aliuziwa kwa Sh.milioni 50 bila kufuata utaratibu.
Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kata ya Mtipa, Abdallah Makiya, akizungumza na waandishi wa habari alisema kuna
kikundi ambacho kimeendelea kudanganyana kuhusu kiwanja hicho na kumwaminisha
mfanyabiashara huyo kuwa atarejeshwa umiliki licha ya kuwepo kwa maamuzi
yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Jelly Silaa.
Alisema Bakwata inatambua kuwa serikali ipo
makini hivyo kamwe haiwezi kugeuka na kutoa uamuzi mwingine tena tofauti na ule
uliotolewa na Waziri wa Ardhi kwenye mkutano wa hadhara wa Rais Samia Suluhu
Hassan ya kwamba hati ya kiwanja hicho ambacho kilikuwa kimenunuliwa na
mfanyabiashara huyo kwa kutumia nyaraka za kughushi ifutwe.
Makiya alisema Bakwata hivi sasa inasubiria siku
60 zilizotolewa na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Kamishna
Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamimu Hozza kukabidhi hati kwa Bakwata kwa
niaba ya Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) kwa kuwa ndio
wamiliki halali wa kiwanja hicho.
Alisema tatizo kubwa kwa Mkoa wa Singida baadhi
ya viongozi wa dini ya kiislamu wameacha kabisa kufuata misingi ya dini na
badala yake wanaendekeza majungu,fitina na umbeya jambo ambalo kimsingi halina
afya kwa dini na mstakabari wa taifa kwa ujumla.
"Waziri wakati anatolea ufafanuzi wa mgogoro
huu wa kiwanja waziri alisema wazi kwamba viongozi wa taasisi ikiwamo ya dini
hawaruhusiwi kuuza mali bila idhini ya Baraza la Wadhamini,kwa hiyo hata
kiwanja hiki inafahamika waliomuuzia mfanyabiashara huyo kwa njia ya kinyemela
ni baadhi ya viongozi wa dini wakati wanatambua kuwa sheria hairuhusu,"
alisema.
Aidha,taarifa ambazo gazeti hili imezipata ni
kwamba waliomuuzia kiwanja hicho mfanyabiashara huyo wanahaha kutaka kwenda
kumuona rais wakiamini maamuzi yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi Oktoba 16,2023
kwenye mkutano wa hadhara mbele ya rais yatapinduliwa.
Oktoba 16, 2023 Waziri wa Ardhi,Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Silaa, alimwagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa
Singida, Shamim Hoza, kufuta hati ya kiwanja alichouziwa mfanyabiashara Philipo
Masawe maarufu Medikenya kwa zaidi Sh.milioni 50 kwa kutumia nyaraka za
kughushi ambacho kinamilikiwa na Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania
(JUWAKITA).
Alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara
uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhutubia wananchi
mjini Singida wakati wa maadhimisho ya kumbukizi (birthday) ya Mkoa wa Singida
kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake 1963.
Silaa alifikia maamuzi hayo baada kufanya kikao
katika ofisi ya kamishna kusuluhisha mgogoro wa kiwanja hicho namba 2
kitalu A kilichopo eneo la Manga
Manispaa ya Singida ambacho pia kilihudhuliwa na mfanyabiashara huyo na
kubaini aliyemuuzia aliyefahamika kwa jina moja la Abubakari alitumia nyaraka
za kughushi.
Katika
kikao hicho, wanawake wawili Binamu Sagaa na Fatuma Issa waliodaiwa kuweka
saini kwenye muhtasari wa mauziano walikana mbele ya waziri kwamba hawakuhusika
kabisa na kwamba saini zao zimeghushiwa kuhalalisha uuzwaji wa kiwanja hicho.
"Masawe hapa ndugu yangu
unetapeliwa,namwagiza Kamishna wa Ardhi Mkoa Singida kupitia kifungu cha 99 cha
sheria ya usajili wa ardhi afute hati ile uliyokuwa umepewa na atoe hati mpya
kwa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida.
Silaa alisema watu wanapaswa kuwa makini
wasitapeliwa wanaponunua ardhi kwasababu sheria zipo wazi mali zote za taasisi
iwe ya dini au chama haiwezi kuuzwa na mtu binafsi wenye mamlaka ya kuuza mali
husika ni Baraza la Wadhamini na si vinginevyo.
Naye mfanyabiashara huyo katika kikao hicho
alijitetea kuwa hakatai maamuzi ya serikali ya kufutiwa hati ya kiwanja hicho
lakini kwasababu kuna gharama amezitumia kukiendeleza afikiliwe.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo
ya Makazi alimwambia mfanyabiashara huyo kwamba gharama zote alizozitumia amdai
Abubakari aliyemuuzia kiwanja hicho kwa kutumia nyaraka feki.
Aidha,Silaa alimwagiza Sheik wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, kuwatangazia viongozi wake kwamba mali zote za taasisi zinamilikuwa Baraza la Wadhamini hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuiuza bila idhini ya baraza hilo.
Post A Comment: