MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) imesema inayoorodha ya wasanii wote wanaojihusisha na dawa za kulevya na imewataka kuacha mara moja kabla ya kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza leo Novemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari , Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesisitiza wanayo orodha ya wasanii wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa hizo na kwamba muda sio mrefu wataanza kuchukua hatua dhidi yao.
Ametoa maelezo hayo baada ya Wahariri wanaoshiriki Semina iliyoandaliwa na Mamlaka hiyo kutaka kujua ni mkakati gani unachukuliwa katika kuwadhibiti wasanii ambao wengine ni maarufu na wanaonesha kujihusisha na dawa za kulevya waziwazi na wakati mwingine kutumia tungo zao kusifu dawa hizo.
Wakati anajibu hilo Kamishina Jenerali Lyimo amesema sheria inawaruhusu kumkamata mtu yoyote ambaye wanahisi anajihusisha na dawa za kulevya, kwenda kumpima na ikithibitika anatumia basi atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Ameongeza kwamba kwa sasa Mamlaka iko katika mchakato wa kuwa na maabara ya kisasa itakayotumika kupima watu wanaohisiwa kutumia dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua."Tunatarajia kufunga mtambo wa kisasa katika maabara yetu, hivyo tutakuwa na nafasi nzuri ya kukamata wanaohisiwa na kupimwa.
"Pamoja na kuwa na sheria lakini tuliamua kuwa kimya lakini tutakapokamilisha maabara yetu tutaanza kuchukua hatua.Mitambo tayari imewasili katika Bandari ya Dar es Salaam na baada ya kukamilisha tutaanza kupima wote wanaohusishwa na dawa za kulevya.
", Imezungumzwa kuhusu wasanii kutumia dawa za kulevya niwahakikishe msanii yoyote ambaye anajihusisha na dawa za kulevya tutamkamata na kumpima katika maabara yetu.
"Orodha ya wasanii wanaotumia dawa za kulevya tunayo na tutakapoanza hatutajali ukubwa wala umaarufu wao.Tunawatahadharisha waache kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, " amesema Lyimo.
Aidha amesema kuwa katika hilo haitashia kwa wasanii peke yao bali na watu wengine wote ambao wanajihusisha na dawa za nao watakamatwa na kupelekwa katika maabara hiyo kwa ajili ya kuchukuliwa vipimo na kama itathibitika kwa namna yoyote ya kutumia dawa za kulevya sheria itachukua mkondo wake.
Post A Comment: