Na.Samwel Mtuwa- Geita

Wananchi wa Mkoa wa Geita wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumaliza mgogoro wa vigingi baina ya Mgodi wa Uchimbaji madini ya dhahabu Geita (GGM) na wananchi wanaozunguka mgodi uliodumu kwa kipindi cha miaka 23 kuanzia mwaka 1999 hadi 2023.


Utatuzi huo umefanyika leo Novemba 13, 2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde katika ziara maalumu ya kikazi na ambapo ameitisha mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya GGM Geita mjini.

Akizungumza na wananchi katika mkutano huo Waziri Mavunde amesema kuwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Hassan inatambua kilio cha wakazi wa Geita kilichodumu kwa miaka 23 ambapo mgogoro umeshughulikiwa kwa asilimia 85 kwa kukamilisha utatuzi wa maeneo nane kati ya kumi na moja yenye mgogoro wa vigingi.



Waziri Mavunde amesisitiza kuwa makubaliano ya mgodi wa GGM na Serikali ni kwamba katika eneo la Samina mgodi umekubali kuachia upande wa Magharibi na upande wa Mashariki wananchi watalipwa fidia kulingana na uthaminishaji utakavyofanyika kupitia wataalamu wa fidia.

 Katika eneo la Katoma mgodi wa GGM umekubali kuliachia eneo lote ambalo limeendelezwa kwa makazi na miundombinu pamoja na kulipa fidia ya usumbufu kwa kipindi cha miaka 23 na Halmashauri kulithaminisha eneo lote kwa wananchi.


Waziri amefafanua kuwa eneo la Kampaundi na Nyanza , mgodi umekubali kuyaachia maeneo hayo na kuyarudisha kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo kama Serikali ilivyopendekeza katika kikao cha awali na mgodi.

Katika eneo la Mgusu na Manga Mgodi umekubali kuyaachia maeneo hayo kwenda kwa wananchi pamoja na leseni ya mgodi kufanyiwa marekebisho ya mipaka ili kuweka alama za kudumu kati ya mgodi na eneo la makazi ya wananchi. 


Aidha, Waziri Mavunde amewataarifu wananchi kuwa katika maeneo yote yaliyokuwa na mgogoro yamebaki maeneo matatu ambayo Serikali inaendelea na majadiliano ya kisheria ili kupata namna bora ya kutatua ikiwa pamoja na hali ya uthaminishaji na kulipa fidia yenye thamani halisi katika maeneo hayo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu kwa kuwajali wananchi wa Geita katika utatuzi wa mgogoro wa miaka 23 akisema kuwa wananchi wataendelea kuwa na imani na viongozi wake hasa katika kuwaletea maendeleo na kutatua changamoto za migogoro ya mipaka.

*VISION 2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI*

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: