Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi (ACP) George Katabazi ametoa wito kwa waandishi wa habari kutoa elimu kwa jamii kwa kuandika habari na makala ili waache kufanya ukatili wa kijinsia hususani wa kingono na wasijichukulie sheria mkononi.

Kamanda Katabazi ameyasema hayo mjini Babati kwenye mdahalo wa ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, uliondaliwa na shirikisho la vilabu vya waandishi wa habari nchini UTPC na kuhusisha klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara (MNRPC) na polisi.

Amesema waandishi wa habari wana uwezo mkubwa wa kutumia taaluma yao ili kutoa elimu kwa jamii hivyo kupitia redio, TV, magazeti na mitandao kukemea hayo.

Amesema matukio ya ukatili wa kijinsia hasa wa kingono na watu wanaojichukulia sheria mkononi yanakuwa yanatokea mara kwa mara hivyo yanatakiwa kukemewa.

Hata hivyo, kamanda Katabazi amesema askari polisi wanne wamefukuzwa kazi kwa makosa ya kupokea rushwa na utovu wa nidhamu wakati wakiwa kwenye utendaji kazi wao.

Akizungumza bila kuwataja majina askari hao wanne, kamanda Katabazi amesema polisi imewafukuza kazi hivi karibuni kwa makosa ya kupokea rushwa na utovu wa nidhamu.

Mkurugenzi mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya amesema mdahalo huo umelenga kuendeleza ushirikiano kati ya polisi na waandishi wa habari katika kuitumikia jamii bila mikwaruzo kwani wanategemeana.

Simbaya amesema waandishi wa habari wanawajibika kwa jamii siyo kwa viongozi hivyo ni muhimu kushirikiana na polisi ili waweze kutimiza wajibu wao kwa amani.

Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara, (MNRPC) Zacharia Mtigandi amempongeza kamanda Katabazi kwa namna anavyoshirikiana na waandishi wa habari hasa katika kutoa taarifa za matukio mbalimbali.

Ofisa program, mafunzo, utafiti na machapisho wa UTPC, Victor Maleko amesema mdahalo kama huo utafanyika tena wilayani Kiteto na kuhusisha polisi na waandishi wa habari.

Share To:

Post A Comment: