MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe Scholastica Kevela amempongeza Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika  Oktoba 27,2023 jijini Luanda nchini Angola.


Dkt. Ackson amechaguliwa kwa kupata kura 172 kati ya kura 303 zilizopigwa na kwa hatua hiyo  anarithi mikoba ya Rais aliyemaliza muda wake, Duarte Pacheco kutoka Ureno aliyekuwa Rais wa IPU kwa mihula mitatu.

Dkt. Tulia anakuwa rais wa 31 wa IPU na mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushika wadhifa huo na katika kusisitiza hilo Mwenyekiti huyo wa WUT Njombe amesema hatua hiyo ameiletea sifa kubwa nchi  Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Amesema kitendo cha Dk Tulia kushinda wadhifa huo akiwa mwanamke wa kwanza, kutazidi kulitangaza Taifa na kuliletea heshima kubwa katika mataifa mengine kwa kuifanya iendelee kufuatiliwa huku akiwataka watanzania wote kumuombea ili aweze kuitumikia nafasi hiyo kwa weledi.

"Dk Tulia ameonyesha Wanawake tunaweza, Tanzania inaongozwa na Rais Mwanamke na upande mwingine Dk Tulia anaenda kuongoza Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) hiyo ni ishara tosha kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na viongozi wanawake wenye kipawa kikubwa Cha uongozi " amesema Mama Kevela.

Asema wao kama Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe na nchi nzima kwa ujumla watampa kila aina ya ushirikiano anaouhitaji ili kuhakikisha nafasi aliyoipata anaitendea kazi kwa ukamilifu mkubwa katika kipindi chote cha uongozi wake.

Dkt Tulia anakuwa Rais wa 31 kuongoza chombo  hicho kinàchoundwa na maspika na Wabunge kutoka nchi120 Duniani ambapo katika miaka 25 iliyopita nafasi ya Urais wa IPU imekaliwa na  Wabunge kutoka mataifa ya Misri, Hispania, Chile, India, Italia ,Namibia, Morocco, Mexico, Bangladesh na Ureno na kwa sasa Tanzania.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa wanasema kwa hatua hiyo uteuzi huo wa Dkt Tulia kuwa Rais wa IPU mbali na kulitangaza Tanzania kimataifa pia kutaongeza ushirikiano na mahusiano ya Tanzania na mataifa mengine kutokana Dkt Tulia kuwa mzawa wa taifa hili.

"Hiyo ni sifa kubwa kwa nchi yetu inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Dunia sasa macho yao yote kwetu, tuna Rais wa nchi mwanamke na sasa Rais wa IPU mwanamke, tunastahili pongezi hakuna ubishi kuwa wanawake tunaweza" ameongeza Mama Kevela

Julai 30 Mwaka huu ,Jumuiya ya Umoja wa Africa(AU) walilidhia kwa kauli moja jina la Dkt Tulia Akson kuwa mgombea wao katika Umoja wa Mabunge Duniani.

Share To:

Post A Comment: