Muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania umezindua rasmi kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili ikiwa na lengo pa kutoa elimu kwa jamii pamoja na kufikiri namna bora za kutatua changamoto mbalimbali zitokanazo na ukatili wa kijinsia hasa katika kundi la wanawake na watoto.
Akizindua kampeni hiyo mjini Morogoro mkurugenzi mtendaji wa UTPC Ndg Keneth Simbaya amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijisia hasa kwa wanawake na watoto ni miongoni mwa ukiukwaji mkubwa uliokithiri wa haki za binadamu na kuwataka wanahabari kushiriki vyema katika kuielimisha jamii hasa juu ya sera, sheria pamoja miongozo ambayo itasaidia kuleta mabadiliko na kupunguza ama kuondoa kabisa ukatili.
"Waandishi wa habari kemeeni vitendo vya ukatili kwa kuandika na kuibua kila aina ya vitendo vinavyosababisha ukatili, na sii hivyo tu badala yake pia iwe sanjari na kutoa elimu kwa kuandaa vipindi pamoja na kuzipa habari zihusuzo ukatili katika vyombo vyetu vya habari". Alisema mkurugenzi.
Naye Lilian Lucas mjumbe wa bodi ya UTPC ambaye pia alimwakilisha rais wa klabu hiyo amesema kuwa baada ya kuzindua kampeni hii ni jukumu la wanahabari kutambua kuwa wanao mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko katika jamii ikiwemo kutokomeza vitendo vya ukatili.
Kupitia kampeni hiyo, UTPC itatumia siku hizo 16 katika kutoa elimu ikiwemo kuandaa mada na mijadala mbalimbali ikiwemo ndoa na mimba za utotoni, ukeketaji na vitendo vingine kama hivyo ambavyo vimekuwa na madhara makubwa na wakati mwingine hata kugharimu maisha ya watu.
Kwa mwaka huu kauli mbiu ni Wekeza, zuia ukatili wa kijinsia.
Post A Comment: