KATIKA kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Arusha imefuatilia na kukagua miradi 21 ya maendeleo na miradi miwili imekutwa na viashiria vya ubadhilifu wa jumla ya Sh milioni 10.8
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa mkoani hapa, Zawadi Ngailo alisema kuwa viashiria vya ubadhilifu vimebainika katika miradi ya miwili ya elimu katika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Ngailo alisema kuwa tayari taasisi yake imeshafungua majalada mawili ya uchunguzi dhidi ya wahusika na uchunguzi ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.
Alisema Takukuru ilikagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo 21 yenye thamani ya Sh bilioni 15.7 na miradi 19 ilikutwa na mapungufu ikiwemo ucheleweshaji wa miradi kukamilika pamoja na kasoro katika ujenzi.
Zawadi alisema kuwa hatua ilizochukuwa taasisi yake katika miradi hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wadau na kufanya vikao vya utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na kuboresha mapungufu na kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.
Alisema katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba mwaka huu Takukuru ina mkakati wa kuendelea kutekeleza programu ya Takukuru Rafiki ili kuwapa Wananchi fursa ya kushiriki katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili katika meneo yao.
Zawadi alisema kuwa programu hiyo imetekelezwa katika kata 13 ambapo jumla ya kero 14 zilibuliwa na kero 29 ziliweza kupatiwa ufumbuzi.
Alisema pia ofisi yake imejipanga kushirikiana na ofisi ya Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Kanda ya Kaskazini kuelimisha vijana kupitia klabu za wapinga rushwa juu ya madhara ya rushwa na dawa za kulevya katika maendeleo yao ya kitaaluma na maisha kwa ujumla.
Alisema kazi hiyo ni utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa baina ya Takukuru na Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti dawa za kulevya nchini na Takukuru itaendelea kufuatilia matumizi ya fedha za serikali zinazoelekezwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika ngazi ya kata,mtaa na vijiji ili kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kama zilizokusudiwa.
Aidha Takukuru mkoani Arusha inaendelea na jukumu la uchunguzi wa malalamiko ya vitendo vya rushwa yaliyopelekwa katika taasisi hiyo kwa njia mbalimbali katika kipindi hicho jumla ya taarifa 146 zilipokelewa ambapo taarifa za rushwa 125 na zisizo za rushwa 21.
Post A Comment: