Na John Walter-Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amezindua mradi wa maji kijiji cha Mewadani wilayani Mbulu, wenye thamani ya shilingi milioni 774,845,160.00.
Mradi huo wenye tangi la ujazo wa lita 225,000 ni muendelezo wa azma ya serikali ya awamu sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji na badala yake wajikite kwenye shuguli zao za uzalishaji.
Akizungumza na wakazi wa Mewadani mara baada ya kuzindua mradi huo Mkuu wa mkoa amesema mradi uliozinduliwa ni mojawapo ya malengo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaondolea wananchi adha ya kukosa maji.
“Rais wetu ameendelea kutoa fedha nyingi za miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi hawapati shida ya maji na hii ahadi aliitoa akiwa makamu wa Rais,”
Mkuu wa Mkoa pia amewataka wananchi wenye uwezo kuunganisha maji majumbani wafanye hivyo ili kupata huduma hiyo kwa ukaribu zaidi na kutumia muda wao kufanya shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Meneja wa wakala wa maji Vijijini (RUWASA) wilaya ya Mbulu Mhandisi Onesmo Mwakasege ameeleza kuwa pia wamejenga vituo 47 vya kuchotea maji, kuzungusha fensi eneo la chanzo na tenki na kufikisha maji kwenye taasisi zote zilizopo kijiji cha Mewadani.
Mwakasege amesema mradi huo unawahudumia wakazi 4,250 wa kijiji hicho sawa na asilimia 65.
Mkazi wa Mewadani Michael Gewe amesema ni fura kwao kupata maji kwani kabla ya mradi huo walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 6 kufuata maji kwenye makorongo.
Wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwasogezea huduma muhimu za kijamii hususani maji na kwamba magonjwa ya kuharisha yaliyokuwa yanawakumba kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama yamekwisha.
Post A Comment: